Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amekabidhi zawadi katika Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Jerusalem Home of God’s Love For Children kilichopo Kimara jijini Dar es salaam. Zawadi hizo ni pamoja na vyakula, vinywaji, sabuni, mafuta ya kupikia pamoja na mavazi.
Akikabidhi zawadi hizo Msaidizi wa Sheria wa Makamu wa Rais, Bw. Elisha Suku amesema Makamu wa Rais ametoa zawadi hizo kwa lengo la kusheherekea pamoja na watoto hao sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya. Aidha ameongeza kwamba Makamu wa Rais amewatakia heri na afya njema watoto pamoja na walezi wao.
Akizungumza mara baada ya kupokea zawadi hizo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kimara jijini Dar es salaam, Wilbroad Matsai amemshukuru Makamu wa Rais kwa zawadi hizo pamoja na viongozi wote wanaojitoa kwa ajili ya kusaidia wenye uhitaji.