Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Aagiza Kuwekwa Utaratibu wa Kupima Matokeo ya Huduma Wanazotoa Maafisa Ugani
Aug 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameiagiza TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara za sekta za Kilimo, Misitu, Mifugo na Uvuvi kuweka utaratibu wa kupima matokeo ya huduma wanazotoa Maafisa Ugani hapa nchini ili kuimarisha utendaji kazi wao utakaopelekea kuinua sekta ya kilimo hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane 2022 kitaifa yanayofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya. Amesema Maafisa Ugani hawapaswi kukaa maofisini bali kuwatembelea wakulima pamoja na wao wenyewe kuwa na mashamba darasa ili waweze kutoa elimu kwa vitendo na sio nadharia tu.

Halikadhalika, Makamu wa Rais ameongeza kwamba taasisi za tafiti hapa nchini zinapaswa kujiongeza na kutafiti mbegu ambazo zinazaa zaidi na mazao mapya yanayostawi vizuri katika kila mkoa pamoja na kuziasa taasisi za umma na binafsi kuweka nguvu zaidi katika kubuni mashine kwa ajili ya kusindika na kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa taasisi za fedha hapa nchini kuendeleza jitihada za kuweka masharti nafuu ya upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuongeza uwekezaji na uzalishaji katika sekta hizo na kupunguza changamoto za ajira. Aidha, amelitaka Shirika la Bima la Taifa kuweka nguvu na kuelimisha wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu faida ya kuwa na bima ya mazao.

Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kujipanga vizuri kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha mbolea ya kutosha pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa mbolea ambapo tayari Wizara ya Kilimo imetenga Shilingi bilioni 150 ili kuanza kutoa mbolea ya ruzuku.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema serikali imedhamiria kujenga Barabara ya njia Nne (Km 29) kuanzia Uyole (Nsalaga) hadi Ifisi pamoja na kujenga barabara ya mchepuko kutoka Uyole hadi Songwe (Km 48.9) itakayowezesha magari makubwa ya mizigo kupita kwenda nchi jirani na mikoa inayopakana na Jiji la Mbeya ili kuboresha miundombinu pamoja na kukabiliana na changamoto ya ajali za mara kwa mara mkoani humo.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali inaendelea na maboresho ya sekta ya kilimo hapa nchini ikiwemo kutoa ruzuku, kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, kujenga miundombinu ya uhifadhi wa mazao pamoja na kuwekeza katika ugani. Amesema kwa sasa Tanzania inauza mazao ya chakula ikiwemo mchele katika Jumuiya ya Ulaya kutokana na uwekezaji na uwekaji wa mazingira mazuri ya biashara hapa nchini.

Aidha, Waziri Bashe amesema Serikali haitafunga mipaka katika biashara ya mazao na kuwahakikishia watanzania uwepo wa chakula cha kutosha katika hifadhi ya taifa chakula hapa nchini na kuahidi kupelekea mazao ya chakula katika maeneo yatakayoathirika na bei za mazao hayo

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi