Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamishna wa Tume Utumishi wa Umma Wafanya Ziara DUWASA
Sep 30, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Hamisa Kalombola ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuendelea kuwa wabunifu ili kuhakikisha majisafi na salama yanapatikana wakati wote.

Ameyasema hayo jana wakati wa ziara ya kikazi ya makamishna wa tume hiyo katika ofisi za DUWASA ambapo alizungumza na menejimenti ya Mamlaka hiyo.

“Mamlaka yenu iendelee kufanya tathmini ya mipango yake ili uwekezaji unaofanyika uwe na matokeo chanya na lengo la Serikali la kuwaletea Watanzania ustawi wa maendeleo liweze kufikiwa,” alisema Jaji Mstaafu Hamisa

Pia, aliwataka Watumishi kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu, uzembe, wizi, ubadhilifu, uombaji wa rushwa ili wananchi wapate huduma bora.

“Mtaweza kujiepusha kutenda makosa kwa kuhakikisha wakati wote mnatekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu,” alisema Jaji mstaafu Hamisa

Naye Kamishina wa Tume hiyo, Susan Mlawi alisema wao kama tume wana jukumu la kuweza kufahamu mazingira ambayo watumishi wanafanya kazi ikiwa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma zinazingatiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema kwa sasa miradi ambayo inahitajika kutekelezwa kwa uharaka ni kupeleka maji mjini Dodoma kwa kutumia bwawa la Mtera wakati ikisubiriwa maji ya Bwawa la Farkwa au ziwa Victoria ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu.

Alisema mahitaji ya maji kwa Jiji la Dodoma ni lita milioni 133 kwa siku lakini yanayozalishwa kwa sasa ni lita milioni 67 hivyo kuna upungufu wa lita milioni 66 lakini mradi wa maji kutoka Bwawa la Mtera unatarajia kuingiza lita 68 na kufanya Jiji liwe na lita 201 milioni ambayo yatatosha kwa matumizi walau kwa miaka 13 ijayo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi