Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamishna wa Ardhi Walioshindwa Kutoa Taarifa ya Uhakiki Mashamba Watakiwa Kujitathimini
Sep 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa nane nchini kujitathimi kutokana na kushindwa kutoa taarifa ya uhakiki wa mashamba katika muda uliopangwa.

Waziri wa Ardhi aliagiza ufanyike uhakiki wa mashamba na kupatiwa taarifa ifikapo Julai, 2022  ambapo Katibu Mkuu aliongeza muda huo hadi Agosti 15, 2022 taarifa hizo ziwe zimewasilishwa.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 6 Septemba, 2022 wakati wa kikao kazi cha Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa 26 nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaaam.

Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wanaotakiwa kujitathmini ni kutoka mikoa ya Arusha, Dodoma, Geita, Kagera, Njombe, Shinyanga, Simiyu na Songwe. Hadi wakati Dkt. Mabula anakutana na Makamishna ni mikoa 17 pekee iliyowasilisha taarifa za uhakiki wa mashamba

Aidha, Waziri wa Ardhi ameonesha kutofurahishwa na utendaji kazi wa Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa ya Rukwa na Simiyu na kuelekeza kuondolewa katika nafasi yake kamishna wa  Mkoa wa Rukwa, Swagile Juma.

Pia, alionesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wizarani, Bw. Venance Mworo na kuelekeza Mkurugenzi huyo kuhamishwa Wizarani kutokana na kushindwa kwenda na kasi ya ubadilishaji mifumo ya TEHAMA hasa ikizingatiwa wizara kwa sasa iko katika mabadiliko makubwa ya kwenda katika mifumo ya kidigitali.

‘’Mhe. Rais ameelekeza kazi ziende kwa kasi kubwa na sasa tunaingia katika mfumo wa kidigitali ambapo tumeanza katika kasi hii lakini tunaye Mkurugenzi wa TEHAMA ambaye ameshindwa kuendana na kasi ya Mhe. Rais’’ alisema Dkt. Mabula.

 ‘’Hili haliwahusu ninyi pekee, nataka ujumbe uwafikie wataalamu wote wa sekta ya ardhi kuwa tunachukua hatua ili kuhakikisha tunaimarisha utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea’’, alisema Dkt. Mabula

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, Makamishna Wasaidizi wameteuliwa kwa utaratibu na kwa hati maalum zinazowaelekeza kusimamia shughuli zote za sekta ya ardhi kwenye ngazi ya Mikoa  na Halmashauri kwa niaba ya wizara.

‘’Wapo baadhi yeu mna mapungufu ya kuelewa nini mnapaswa kufanya, mnakosa weledi na ubunifu, mnafanya kazi kwa mazoea, mnaogopana, mnalindana na kuathiri utendaji wetu wa kazi’’, alisema Dkt. Mabula.

Alieleza kuwa, pamoja na hatua za kinidhamu ambazo wizara imekuwa ikizichukua kama vile kuwaachisha kazi baadhi ya watumishi wa Mikoa ya Mbeya na Dodoma aliagiza hatua zichukuliwe kwa watumishi wa mikoa mingine na kubainisha mikoa ambayo wizara inakamilisha hatua za kinidhamu za kuchukua hivi karibuni kuwa ni ile ya Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha pamoja na Lindi.

Aidha, Waziri Dkt. Mabula alielezea pia ongezeko la ujenzi holela katika miji na hivyo kuathiri ukuaji uendelezaji wa miji ambapo alitolea mfano uwepo wa ujenzi wa vituo vya mafuta alioueleza kuwa unafanyika bila udhibiti na utaratibu na kuagiza kusimamiwa ipasavyo na kwa nguvu zote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula alisema, Wizara ya Ardhi inashindwa kufikia matarajio ya wananchi kutokana na baadhi yao kukata tamaa kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi.

‘’Baadhi ya wadau wetu wamekata tamaa kwa kuwa wanaamini ili kupata huduma kutoka wizarani kwetu ni lazima uwe na mtu au utoe rushwa, kwa hiyo tumejipanga kufanya mabadiliko makubwa ili kurejesha imani kwa wateja wa wizara’’, alisema Dkt. Kijazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi