Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majiji Manne kufungwa Kamera za Usalama
Aug 28, 2023
Majiji Manne kufungwa Kamera za Usalama
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza wakati wa Mkutano wa Kuwajengea Uwezo Wakuu wa Mikoa yote na Makatibu Tawala, mkutano uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu

Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi katika kudhibiti matukio ya uhalifu na makosa ya usalama barabarani kwa kufunga kamera maalumu katika majiji ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha huku lengo likiwa kufunga kamera hizo katika mikoa yote nchini kwa siku zijazo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa Mkutano wa Kuwajengea Uwezo Wakuu wa Mikoa yote na Makatibu Tawala, mkutano uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

 

“Katika kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi letu la Polisi kuna maeneo muhimu sana tumeamua kuyapa kipaumbele, moja ni kujenga mazingira mazuri ya Askari wetu kufanya shughuli zao ikiwemo makazi yao, vitendea kazi zao, matumizi ya mifumo na teknolojia za kisasa katika kubaini, kukabili, kushughulika na kudhibiti uhalifu, nichukue fursa hii kuutambulisha kwenu Mradi mkubwa wa Mji Salama, kutokana na juhudi za Mhe. Rais kuimarisha demokrasia ya uchumi tumeweza kupata mkopo wenye masharti nafuu unakuja kutusaidia kusimika mradi wa kimkakati wa mji salama”, alisema Waziri Masauni.

 

“Na Miji ambayo tutaanza nayo ni Mji wa Kibiashara Dar es Salaam, Makao Makuu ya nchi Dodoma, Makao Makuu ya kitalii Arusha pamoja na Jiji la Mwanza huku mradi huo ukienda sambamba na Mradi wa Ukaguzi wa Lazima wa Magari na Mradi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Dar es Salaam”, aliongeza Waziri Masauni.

 

Katika mkutano huo, Waziri Masauni alitaja maeneo mengine ya vipaumbele kwa Jeshi la Polisi ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi kuwa ni kuendelea kudumisha usalama wa raia na mali zao kwa kufanya doria, misako na operesheni maalumu katika mipaka, maziwa makuu na Bahari ili kudhibiti uhalifu nchini na kupunguza matishio ya uhalifu, makosa makubwa ya jinai na ajali za barabarani.

 

Ametoa rai pia kwa jamii kuendelea kushirikishwa katika masuala ya ulinzi kupitia kitengo cha polisi jamii, kuimarisha uweledi wa Maafisa, Wakaguzi na Askari kupitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi sambamba na kuhudhuria mikutano ya kanda, kikanda, kimataifa pamoja na operesheni za kimataifa ili kuboresha huduma za polisi nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi