Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa: Tanzania Kuwa Wazalishaji Wakubwa wa Nishati
Sep 20, 2023
Majaliwa: Tanzania Kuwa Wazalishaji Wakubwa wa Nishati
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Nishati kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 20, 2023.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Septemba 20, 2023 amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na kusema kwamba Serikali imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na nishati.

“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi.“

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Nishati kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba  20, 2023. 

Amesema kuwa Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua.

Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha  viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzisisitiza nchi zote wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa  programu maalum za mafunzo katika sekta za nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye sekta hiyo.

Amesema kuwa nishati ni sekta muhimu katika kufikia lengo la uanzishwaji wa viwanda na katika kuimarisha na kuwezesha uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi. “Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili kufungua fursa kwa Watanzania wote.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakimsikiliza Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa Gesi ya SONGAS, Dkt.  Michael Mingodo (kulia) wakati alipotembelea banda la maonesho la kampuni hiyo baada kufungua Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Nishati kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba  20, 2023.

Amesema ili kuwaendeleza wafanyabiashara wa ndani na Watanzania kushiriki katika sekta ya nishati, Serikali itaendelea kuhakikisha kanuni na taratibu zinazofaa zinawekwa ili kuwezesha ushirikishwaji katika mnyororo wa thamani wa maendeleo kwenye sekta ya nishati

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliyojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.

Dkt. Biteko amesema zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa nishati.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi