Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi, mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya msingi Ng’au, iliyopo kata ya Mnacho Wilayani Ruangwa, Novemba 5, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wilaya ya Ruangwa inahitaji kuwa na shule ya sekondari ya wasichana ambayo ni ya bweni ili kupunguza tatizo la wasichana kukosa elimu.
Ametoa wito huo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ng’au, kata ya Mnacho wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambako alienda kukagua ujenzi wa shule mpya ya msingi ambayo ujenzi wake ulianza wiki mbili zilizopita.
“Mpango wetu ni kujenga shule ya msingi mpya hapa kijijini Ng’au ili watoto wanaotoka ng’ambo hii wasome hapa hapa. Wakati wa masika nyote mnajua taabu wanayopata watoto wetu kukatisha kwenda ng’ambo ile,” alisema.
“Nimefurahi kukuta msingi wa vyumba tisa uko tayari na hii idadi inaweza kuongezeka. Wanakijiji tushirikiane kujaza kifusi ili kazi ya ujenzi iende haraka,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ng’ambo ya pili kuna shule ya msingi Mnacho ambayo ina madarasa 11 na wanafunzi waliopo ni karibu 500, na ndoto yake ilikuwa ni kuona ile shule inabadilika na kuwa ya sekondari.
“Ile shule ina historia na wakazi wengi kutoka Nandagala, Namahema, Chimbila ‘A’ na Chiemeka wamesoma pale. Mimi mwenyewe nimesoma pale kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. Shule ilishazeeka, ndipo tukatafuta fedha ili ifanyiwe ukarabati na sasa ina miundombinu mizuri ndiyo sababu inaonekana inafaa kuwa ya sekondari,” alisema.
“Kwa vile shule ina miundombinu ya kutosha, ni vema ikawa ya bweni ambayo ni mahsusi kwa wasichana wa wilaya hii kwani tunalo tatizo la watoto wa kike kupata elimu, na wanahangaika sana,” alisema.
“Ujenzi wa hii shule ukikamilika, watoto wale 500 watahamia hapa na walimu wao na ile pale itapokea wanafunzi sekondari za wilaya hii ili tuwe na kidato cha kwanza hadi cha nne na ianze mara moja,” alisema.
Alisema shule hiyo itaitwa Lucas Malia kwa heshima ya mwalimu mkuu wa zamani wa shule hiyo ambaye alisomesha watu wengi katika wilaya hiyo na wengine sasa hivi ni viongozi Serikalini na jeshini. Mwalimu Malia hivi sasa ni marehemu.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma leo asubuhi kuendelea na vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho (Jumanne, Novemba 7, 2017).