Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa: Nimefurahishwa na Utekelezaji wa Agizo la Rais, Dkt. Samia
Dec 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

*Ni la kudhibiti tembo wanaovamia makazi na mashamba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa amefarijika kuona Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) imeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwadhibiti Tembo wanaovamia mashamba na makazi ya wanananchi kwenye wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa katika Mkoa wa Lindi.

Amesema hayo leo (Desemba 2, 2022) wakati alipopewa taarifa ya zoezi hilo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI),  Dkt. Elbate Mjingo kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea mkoani Lindi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia alipohutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba 01, 2022 kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuwatumia watalaamu wake kutekeleza agizo la kuwadhibiti tembo wanaovuka mipaka ya hifadhi na kuvamia makazi na mashamba ya wananchi.

Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza kamati za ulinzi na usalama kwenye wilaya hizo kutoa elimu kwa wananchi juu ya utekelezaji wa zoezi hilo ikiwa pamoja na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ili kutosababisha wanyama kurudi kwenye maeneo ya makazi na mashamba.

“Tahadhari zitolewe, wananchi wanapaswa kukumbushwa mara kwa mara ili mazoezi ya udhibiti wa wanyamapori na utoaji wa elimu yaende pamoja”.

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Dkt. Elbate amesema kuwa wamebaini uwepo wa makundi manne ambayo kati ya hayo matatu yapo Wilaya ya Nachingwea na moja lipo Wilaya ya Liwale.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu Kundi moja lina tembo 50, lingine tembo 20, lipo lenye tembo 5 na lipo la tembo 7, tumevalisha mkanda kwenye kundi moja la tembo na mengine tunatarajia kuyavalisha leo ili tuweze kufuatilia nyendo za kila kundi”

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi