Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa: Maambuzi ya Covid-19 Yamepungua Nchini
Jun 16, 2020
Na Msemaji Mkuu

  • Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa amesema maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) kwa sasa yamepungua na idadi ya wagonjwa waliopo nchini hadi leo ni 66.

    “Anayestahili sifa katika hili ni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa msimamo wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo ambayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa nchi.”

    Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) wakati akihitimisha shughuli za Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma. “Mheshimiwa Rais ameifanya Tanzania iwe ya kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu”.

     Waziri Mkuu amesema “nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za bara la Afrika zilichukua hatua kadhaa za kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao (Lockdown), kuzuia mikusanyiko kwa kufunga shule, vyuo, michezo, aina zote za usafiri wa ndani na nje, maeneo ya ibada na shughuli za uzalishaji mali na viwanda vilifungwa.”

     Waziri Mkuu aliongeza kuwa Tanzania ilianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na maambukizi kwa kuunda Kamati tatu za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi. Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza misongamano kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

     “Siku ya tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akiwa Jijini Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020 akiwa Chato aliwataka Watanzania wawe watulivu waondoe hofu ya ugonjwa huu na waone ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu na akawataka Watanzania wachukue tahadhari na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani na kutofunga nyumba za ibada.”

     Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo na kusisitiza mambo matano ambayo ni pamoja na kuwasihi Watanzania kuondoa hofu kwa kuwa Mwenyezi Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.

     Pia, aliwataka Watanzania watumie siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nao na atawasikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji kutoka pande mbalimbali za dunia.

     Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli aliwahimiza Watanzania wamtegemee Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayewavusha na kuwaepusha na janga hilo. Pia, aliwahimiza Watanzania kutopuuza umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19. “Kauli hii, imekuwa chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19”. Amesema Waziri Mkuu.

     Vilevile, Waziri Mkuu amesema Mei 20, 2020 akiwa Singida, Rais Dkt. Magufuli aliwaomba Watanzania watumie siku tatu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu aliyoyafanya kwa Taifa la Tanzania kwa kuliepusha na kusambaa kwa virusi vya COVID-19.

     Amesema suala la kudhibiti maambukizi ya COVID-19 litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa sambamba na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan katika kipindi hiki ambacho WHO imebainisha kwamba si wa kuondoka mara moja watu wajifunze kuishi nao.

     Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Juni 9, 2020 Bunge lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

     “Katika hili, nami naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu ugonjwa huu ambapo alihimiza masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana na janga hili na hivyo, kuondoa hofu na taharuki iliyokuwa imetanda kwa Watanzania.”

     “Leo tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua imepungua sana. Kwa mfano, taarifa ya leo, Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 inaonesha kuwa tuna wagonjwa 66 kutoka katika mikoa 10 huku mikoa mingine 16 ikiwa haina wagonjwa.”

     Pia, Waziri Mkuu ametoa pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na waumini katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote viongozi hao wamekuwa wakiwapatia faraja waumini na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya. “Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.”

     Amesema taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha kuwafungia watu ndani yaani “Lockdown” kitasababisha kusinyaa kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa asilimia mbili kila mwezi.

     “Hivi sasa, nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown” si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili na hata wa tatu.”

     “kwa mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya kuwapongeza Watanzania ambao si tu walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa na mamlaka yoyote ya nchi.”

     Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wa afya kwa usimamizi wa tatizo hilo kwani walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari ya virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao.

     Vievile, Waziri Mkuu ameishukuru sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia wito wa Serikali kwa kutoa michango ya hali na mali katika kufanikisha vita dhidi ya COVID-19 nchini. Pia wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini.

    OFISI YA WAZIRI MKUU,IMETOLEWA NA:

    S. L. P. 980,

    41193 - DODOMA,                      

    JUMATATU, JUNI 15, 2020.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi