Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Kampuni ya Tumbaku ya Japan (JT Group) utakayoiwezesha kampuni hiyo kuendelea kutoa huduma za kijamii katika maeneo inayonunua zao la hilo nchini.
Mkataba huo wa miaka mitatu wenye thamani ya shilingi bilioni 3.2 utaiwezesha kampuni hiyo kutoa huduma hizo kwenye sekta za afya, elimu, maji na uwezeshaji wananchi kiuchumi kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Majaliwa ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo leo Jumatatu, Septemba 11, 2023 kwenye Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya mazungumzo kati yake na kampuni hiyo wakati wa ziara yake nchini Japan Septemba 2022 na Mkutano wa TICAD 8 uliofanyika Agosti 2022 nchini Tunisia.
“Wanataka watumie faida wanayoipata hapa nchini kutokana na biashara yao kuweza kuisaidia jamii, wameamua kuiweka kwenye utaratibu wa kuwa na makubaliano kati yao na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, tayari wameshajenga shule ya wasichana kule Urambo, Tabora, wameshajenga zahanati Uyui, pia wamedhamini vijana kwenye masomo”.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wadau tunaoshirikiana nao wanakuwa na michango ya maendeleo kwenye huduma za jamii kwenye maeneo wanatoa huduma.
Amesema kuwa kupitia mkataba huo kampuni ya JT Group itajenga vituo vya kutolea huduma za afya, shule ya wasichana ya kulala katika moja ya halmashauri wanayozalisha tumbaku pia wataweka miundombinu ya maji safi ili kuongeza upatikaji wa huduma hiyo kwenye maeneo wanayouza tumbaku. “Kampuni imetoa ajira zaidi ya 450 kwa watanzania kwenye maeneo wanayonunua tumbaku”
Naye Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya JT Group Masamichi Terabatake amesema kuwa kampuni ya JP Group inanunia tumbaku ya kijani katika nchi takribani 35 na Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazozalisha kwa wingi na ameipongeza Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini.
Mpaka sasa kampuni hiyo imeshajenga Kituo cha afya kilichopo Uyui mkoani Tabora, Shule ya sekondari ya wanawake iliyopo Urambo, maeneo ya kuchotea maji pamoja na kuendesha programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.