Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mahakama Mpya Sita Zinazotembea Kuanza Kazi 2024
Oct 24, 2023
Mahakama Mpya Sita Zinazotembea Kuanza Kazi 2024
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desderius Kamugisha akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Arusha wakati akizunguka na Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika katika mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa kwa ajili ya mkutano mkuu wa mwaka wa Majaji Wakuu hao (SEACJF) unaoendelea jijini humo.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Mahakama Kuu ya Tanzania imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuongeza mahakama mpya sita zinazotembea ambazo zinatarajiwa kuanza kazi Januari, 2024.

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desderius Kamugisha ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2023 wakati akizunguka na Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika katika mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa kwa ajili ya mkutano mkuu wa mwaka wa Majaji Wakuu hao (SEACJF) unaoendelea jijini Arusha.

"Tumewaeleza Majaji Wakuu kuhusu mahakama zetu zinazotembea na namna ambavyo zinafanya kazi na mpango wetu wa kuongeza mahakama zingine sita zinazotembea ambazo kufikia Januari, 2024 zitaanza kufanya kazi, wamevutiwa sana kuona huduma hizi zinawalenga wananchi ambao hawana uwezo wa kusafiri muda mrefu, wanawake wajane, wananchi waliodhulumiwa, pia hata huduma ya kuwatafuta wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao ya biashara", alisema Kamugisha.

Ameongeza kuwa, Majaji Wakuu hao wamevutiwa na mambo makubwa yanayofanywa na mahakama ikiwemo dhana ya Vituo Jumuishi pamoja na Kituo cha Masuala ya familia ambapo wamevutiwa na namna ambavyo Mahakama ya Tanzania imeweza kuwakusanya wadau wa haki kwenye jengo moja na ngazi zote za Mahakama.

Vile vile, wamevutiwa na matumizi ya TEHAMA hasa Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri pamoja na mfumo unaokuja unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi Novemba ambapo kupitia mfumo huo, Mahakama inaweza kuona kila kitu kinachendelea nchi nzima ndani ya muda mfupi.

Amefafanua kuwa, Mfumo huo wa Menejimenti ya Mashauri unaruhusu kuona hali ya mashauri, pia kunukuu na kutafsiri mienendo ya kimahakama ambapo teknolojia hiyo imemuondolea Jaji au Hakimu jukumu la kuandika maneno kwa mkono na kutafsiri mwenendo au hukumu kwa njia za kawaida.

Aidha, Majaji Wakuu walioneshwa pia mfumo wa usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao uliotumika sana kipindi cha janga la UVIKO-19 ambapo wananchi na wadau wa Mahakama waliweza kusajili mashauri pasipo kufika Mahakamani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi