Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mahakama kwenda Kidijitali
Jan 17, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_27220" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Msaidizi, Mipango na Bajeti -Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akiongea jambo na Washiriki katika Mafunzo hayo.[/caption]

Na Mary Gwera, Mahakama

Mahakama ya Tanzania imedhamiria kufanya malipo yote ya huduma zake na ukusanyaji wa mapato kielektroniki ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia na kuboresha huduma kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi, Mipango na Bajeti-Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso Januari 16, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) yanayofanyika katika Ukumbi mpya ya Mikutano uliopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kisutu jijini Dar es Salaam.

“Mahakama kama ilivyo kwa Taasisi nyingine za Serikali imejiunga katika Mfumo huu ili kufanya ukusanyaji wa mapato na malipo yote ya huduma za Mahakama Kieletroniki, kwa hiyo ili kuwezesha matumizi ya mfumo huo yameandaliwa mafunzo haya maalum kwa watumiaji katika ngazi mbalimbali za Mahakama kuwapa ujuzi wa kuwawezesha kufanya kazi hii,” alifafanua Bw. Uisso.

Alitaja kuwa kwa kuanzia mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yameshirikisha jumla ya Watumishi 35 wa Mahakama kwa Mkoa wa Dar es Salaam, akitaja watumishi hao kuwa ni pamoja na Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Makarani kutoka Makao Makuu na ngazi zote za Mahakama kwa mkoa huu.

[caption id="attachment_27221" align="aligncenter" width="750"] Washiriki wakifuatilia mada wakati wa mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) yaliyofanyika katika Ukumbi mpya wa Mikutano uliopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kisutu jijini Dar es Salaam.[/caption]

“Tunatarajia kuendelea kutoa elimu hiyo katika mikoa mingine kwa awamu, ili kuiwezesha Mahakama nchi nzima kutumia mfumo huu,” aliongeza Bw. Uisso.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Msaidizi anasema kuwa Mfumo wa sasa unaotumika na Mahakama una changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya Mahakama kutowasilisha ‘bank slip’ kwa wakati, fedha kuingizwa kwenye akaunti ambazo sio za Mahakama.

Bw. Uisso anaongeza kuwa mfumo huu umekuja wakati muafaka kwa Mahakama ambapo kwa sasa ipo katika maboresho ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa kuanzisha ‘e-Judiciary’ ili kuboresha mfumo wa usimamizi wa mashauri na ukusanyaji wa takwimu.

Kwa upande wake Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Fedha na Mipango-Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Fedha, Bi. Penina Henjewele aliwatoa hofu washiriki wa mafunzo hayo kuwa mfumo huo ni rafiki kutumia hivyo wasiwe na wasiwasi katika utekelezaji.

[caption id="attachment_27222" align="aligncenter" width="750"] Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Fedha na Mipango-Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Fedha, Bi. Penina Henjewele akitoa Mada ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) kwa Washiriki wa Mafunzo hayo (hawapo pichani)[/caption] [caption id="attachment_27223" align="aligncenter" width="750"] Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali ‘Government Electronic Gateway (GEPG) yaliyofanyika katika Ukumbi mpya wa Mikutano uliopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kisutu jijini Dar es Salaam.[/caption]

“Mfumo huu ni rafiki sana kutumia, vilevile unaokoa muda hivyo basi msiwe na wasiwasi mtaelewa na kufanya vizuri cha msingi ni kufuata taratibu na maelekezo yanayokuwa yakitolewa,”alisema Bi. Henjewele.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yanaendeshwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Mfumo huu wa ‘GEPG’ uliandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wadau wengine.

Tayari Mfumo huo umeshaanza kutumiwa na baadhi ya Taasisi za Serikali kama Wizara ya Ardhi, Wakala wa Misitu, Jeshi la Polisi-Kitengo cha Usalama Barabarani ‘Traffic’ na baadhi ya Halmashauri za Serikali za Mitaa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi