Na Mwandishi Wetu - DODOMA
Jeshi la Magereza nchini huenda ikawa ndio Taasisi ya kusambaza mbegu nchini hivyo kupunguza gharama ya kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwenye uzinduzi wa majengo ya Ofisi Kuu ya Jeshi la Magereza iliyopo Msalato jijini Dodoma.
“Mna mradi wa kuzalisha mbegu pamoja na shamba la michikichi, Magereza inaweza ikawa ndio Taasisi ya kusambaza mbegu Tanzania nzima, litakuwa jambo zuri kwa sababu mbegu zitakuwa ni zetu tofauti na za kuletewa ambazo ukizipanda zinaweza zisiote” ameeleza Mheshimiwa Rais
Pamoja na hayo, Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano italiwezesha Jeshi hilo ili liweze kukamilisha mradi huo wa kimkakati.
“Nchi yetu inatumia fedha nyingi kuagiza mafuta kutoka nje kwa takriban shilingi bilioni 443 hadi bilioni 470 kwa mwaka, pia tunaagiza kiasi kikubwa cha mbegu hivyo tutahakikisha tunawawezesha ili kukamilisha miradi hiyo ya kimkakati” ameongeza Mheshimiwa Rais.
Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema tayari Jeshi hilo limeshasajiliwa kama mzalishaji mbegu huku akimshukuru Rais Magufuli.
“Tunakushukuru Mhe. Rais kwa kutujali kwenye upande wa magari, leo umeyaona magari tisa ambayo umetupatia kwa ajili ya kufanyia kazi, tunakushukuru na tunaomba uendelee kutukumbuka katika hilo” amesema Meja Jenerali Mzee.