Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mafuta Hayajashuka Bei katika Soko la Dunia, Tanzania Tumeshusha Bei
Aug 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Zuena Msuya, Njombe

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imekuwa ikitenga fedha maalum kila mwezi ili kupunguza gharama za mafuta kwa watumiaji kutokana na bidhaa hiyo kuendelea kupanda bei katika soko la Dunia.

Byabato alisema hayo wakati akisalimia wananchi kwenye Mkutano wa hadhara uliyofanyika katika Uwanja Sabasaba wakati wa Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, mkoani Njombe Agosti 10, 2022.

Wakili Byabato alifafanua kuwa, kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, kwa sababu mbalimbali, Serikali imekuwa ikitenga Shilingi bilioni 100 kila mwezi ili kuwapunguzia wananchi gharama za kununua mafuta hayo.

Aliweka wazi kuwa, fedha hiyo inayotengwa na Serikali imewezesha kupunguza Shilingi 200 hadi 300 katika kila lita moja ya mafuta ya Petroli, na Shilingi 400 kwa kila lita moja ya Mafuta ya Dizeli.

Katika ziara hiyo ya Rais, Naibu Waziri aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Akizungumzia masuala ya nishati ya umeme katika Mkoa huo wa Njombe, Byabato alisema Serikali imetenga fedha za kutosha kuweza kutatua changamoto ya umeme mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kusambaza umeme katika Vijiji na Vitongoji.

Vilevile Wakandarasi wanaendelea na kazi katika maeneo mbalimbali kuhakikisha miradi ya usambazaji wa umeme inatekelezeka wananchi kupata huduma.

Aidha, alieleza kuwa, Serikali imetenga Shilingi bilioni 8 katika maandalizi ya kazi za awali za kutekeleza Mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Ruhuji na Rumakali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi