Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi OR-TAMISEMI, Ismail Chami, akifuatilia mafunzo ya EPICOR 10.2 yalioanza leo kwa Maafisa Manunuzi na Ugavi mkoani Mwanza.
Na: Gladys Mkuchu, PS3
Mafunzo ya siku mbili ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma (EPICOR) toleo la 10.2 kwa Maafisa Manunuzi na Ugavi yameanza rasmi hivi leo mkoani Mwanza yakijumuisha maafisa kutoka halmashauri za mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera, Geita, Mara,Tabora, Simiyu na Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Jijini Mwanza, Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ismail Chami, amesema kuwa washiriki hao wanalo jukumu la kuzingatia mafunzo hayo ambayo ni msingi katika usimamizi wa fedha katika Halmashauri zao.
“Mkurugenzi hawezi kutekeleza majukumu yake iwapo watendaji hawatakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao na ndio maana tumeweza kuwashirikisha Maafisa manunuzi na ugavi kwakuwa wao ni muhimili mkuu katika kusimamia manunuzi katika halmashauri zao,” Aliongeza Ismail.
Baadhi ya Maafisa Manunuzi na Ugavi wakishiriki mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma siku ya kwanza mkoani Mwanza.
Meneja Mradi wa PS3 mkoa wa Mwanza, Pelestian Masai akitoa neno la utangulizi katika Mafunzo ya EPICOR 10.2 kwa Maafisa Manunuzi na Ugavi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa leo Jijini Mwanza.
Kwa upande wake mshauri wa Mifumo ya Fedha wa PS3 Dkt. Aloyce Maziku, amesema kuwa mifumo hii hususani ya fedha inaimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika Halmashauri hivyo ni muhimu mifumo hiyo ikatumika kwa kuzingatia taratibu na mwongozo wa mafunzo hayo.
Naye, Meneja mradi wa PS3 mkoa wa Mwanza, Pelestian Masai ametoa wito kwa washiriki kuzingatia mafunzo hayo na kushiriki kikamilifu ili wasipitwe na hatua yoyote ya mafunzo hayo kwa maslahi ya wananchi wa halmashuri zao na Taifa kwa ujumla.
“Tunaamini mfumo huu utaenda kurahisiha kazi zetu sababu hapo awali taarifa nyingi tulikuwa tunaziandaa kwenye madaftari tu, kama vile mkataba wa manunuzi madogo ‘LPO’ lakini kwa mfumo huu ulioboreshwa tutaweza kuandaa taarifa zote kielektroniki na hivyo itarahisisha sana utendaji wa kazi lakini uhifadhi wa taarifa utakuwa wa uhakika na kutusaidia kufanya marejeo kwa taarifa za nyuma,” amesema mmoja wa washiriki Florence Kyabachubya, Afisa Ugavi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mshauri wa Mifumo ya Fedha PS3 Dkt. Aloyce Maziku akitoa maelezo juu ya mradi wa PS3 katika Mafunzo ya EPICOR 10.2 kwa Maafisa Manunuzi na Ugavi mkoani Mwanza.
(Picha zote na PS3)