Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mafia Wapata Elimu ya Utambuzi na Madhara ya Matumizi ya Dawa na Vipodozi Vyenye Sumu
Oct 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Jumla ya wanafunzi na walimu 5,725 wa shule za sekondari na msingi 14 katika wilaya ya Mafia, mkoa wa Pwani, wamepata mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vipodozi ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wakati wa kununua na kutumia bidhaa hizo.

Katika mafunzo hayo, washiriki walielimishwa kuhusu namna ya kuvitambua vipodozi vilivyopigwa marufuku na kuelezwa madhara ya matumizi ya vipodozi hivyo kwa afya ya mtumiaji.

Mafunzo hayo yaliendeshwa hivi karibuni kwa siku tano na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) ambapo wataalamu wa elimu kwa umma na huduma kwa wateja kutoka Makao Makuu ya Mamlaka hiyo wakishirikiana na ofisi yake ya Kanda ya Mashariki.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia Bw. Erick Mapunda aliwezesha mafunzo hayo kufanyika kwa kuwateua Maafisa Elimu Sekondari na Msingi kushirikiana na TFDA katika kukamiliza zoezi hilo muhimu la kunusuru afya za wananchi.

Washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kuviona baadhi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku na kuelezwa kiini cha marufuku hiyo kuwa ni pamoja na vipondozi hivyo kuwa na viambato sumu vilivyopigwa marufuku nchini vikiwemo madini ya zebaki (Mercury), Cloroquinone, Vinyl Chloride na Misuguano (Steroids) nk.

Wanafunzi na walimu hao walielezwa kuwa ni muhimu wakati wanaponunua dawa na vipodozi kusoma maelezo yake ambayo yanaeleza aina ya viambato mbalimbali vya dawa na vipodozi ili kugundua kama kuna vilivyopigwa marufuku.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa TFDA wa kuelimisha umma kuhusu usalama na ubora wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu shughuli zinazofaywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa.

Mbali ya kugawiwa vipeperushi mbali mbali vinavyoelimisha kuhusu bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo lakini pia washiriki walitakiwa kutembelea tovuti ya Mamlaka hiyo (www.tfda.go.tz) kwa lengo la kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za orodha za dawa na vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Akizungumzia mafunzo umuhimu wa mafunzo hayo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Kaimu Meneja wa Elimu kwa Umma na Huduma kwa Wateja Bw. James Ndege alisema kundi hilo ni muhimu kuelimishwa kwani lina ushawishi mkubwa kwa jamii kubwa na pia lipo katika hatari ya kutumia bidhaa zisizofaa kwa matumizi hivyo kuathiri afya zao kwa kuwa ni la vijana ambao hupenda kuonekana warembo na watanashati wakati wote.

“Tunawalenga wanafunzi kwa kuwa hilo ni kundi kubwa ambalo kama litaelewa vyema suala hili kwa kiasi kikubwa tutaweza kufanikiwa kudhibiti matumizi ya dawa na vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa kuwa mbali wao kuachana na matumizi lakini watasaidia kuwaeleza wazazi na jamii inayowazunguka kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na vipodozi visivyofaa”,  alisisitiza Bw. Ndege.

Bw.  Ndege alieleza kuwa mafunzo hayo yalilenga pia kuboresha mahusiano na kuongeza ushirikiano kati ya TFDA na wadau wake hivyo kufanikisha utii wa sheria bila shuruti na utoaji wa taarifa kuhusu uvunjifu wa sheria.

Katika mafunzo hayo, TFDA ilitoa wito kwa walimu na wanafunzi kutoa taarifa za watu wanaovunja sheria kwa kuuza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu ikiwa ni  vipodozi vilivyopigwa marufuku na kuwahakikishia kuwa suala la usiri kwa watoa taarifa.

“TFDA hufanyia kazi taarifa kutoka kwa wadau kwa usiri mkubwa na kutoa mrejesho hivyo kuhakikisha usalama wa mtoa taarifa ni wenye uhakika” alisisitiza Kaimu Meneja huyo.

Alibanisha kuwa katika mafunzo hayo, washiriki kwa nyakati tofauti wameahidi kufikisha elimu waliyoipata kwa ndugu jamaa na marafiki zao hivyo kusaidia katika jitihada za kulinda afya ya jamii ambayo ni nguvu kazi ya kuleta maendeleo ya nchi.

Shule zote za Sekondari za Mafia zilizofaidika na mafunzo hayo ni  Bweni, Kirongwe, Baleni, Kilindoni, Kitomondo na Micheni. Kwa upande wa shule za msingi, zilikuwa Chemchem, Kilimahewa, Msufini, Kigamboni, Utende, Kilindoni, Mtakatifu Yosefu na Kanga.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi