Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) wamepanda jumla ya miti 300 katika eneo la Shule ya Sekondari Ilazo Extension iliyopo jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo leo Oktoba 03, 2023 ikiwa ni moja ya tukio la kijamii lililopangwa kufanyika kuelekea Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika jijini humo Oktoba 05, 2023, Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bibi Mwantumu Mahiza ameyashukuru Mashirika hayo kwa kuja na wazo hilo pamoja na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kutoa ushauri wa aina ya miti inayotakiwa kupandwa mkoani Dodoma na hasa katika maeneo ya shuleni.
"Shule hii ni shule mpya na ya mfano iliyojengwa na Serikali, hivyo kwa kuwa ni mpya inahitaji kupandwa miti mingi, leo tumepanda jumla ya miti 300. Natoa rai kwa Ofisi ya Wilaya ya Dodoma Mjini kuwa kila mti uliopandwa uendelee kuimarika na kuleta matunda,” alisema Mwantumu Mahiza.
Mwenyekiti Mwantumu ameongeza kuwa kupanda miti katika eneo la shule hiyo itawasaidia Walimu na wanafunzi kupata hewa safi, kivuli na kuboresha mazingira yao, vilevile miti ya matunda itawasaidia kuboresha afya zao. Ametoa ushauri na kuwahimiza wakazi wa Dodoma kila mmoja kwenye makazi yake kujitahidi kupanda miti hususan ya matunda.
Akitoa shukrani zake, Mwakilishi wa Shirika la Green Eco Tanzania, Bw. Stanley Shibuda amesema kuwa shirika hilo linafanya kazi ya kuhamasisha upandaji wa miti na kukataza ukataji wa miti, hivyo kushiriki katika zoezi hilo ni moja ya malengo yao ya kuifikia nchi nzima.
"Tunaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa hamasa kwa wananchi kuendelea kupanda miti mingi ili kuboresha mazingira yetu, katika eneo hili tumepanda miche ya miti 300 huku lengo la upandaji miti kwa Mkoa wa Dodoma likiwa ni miche 1,300", amesema Bw. Shibuda.
Nae Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bw. Nestory Mushi amesema kuwa kazi kubwa wanazozifanya ni za uhifadhi na utunzaji wa mazingira nchini na kupitia vilabu mbalimbali vya mazingira vikiwemo vya mashuleni na vyuoni.
"Shughuli za utunzaji na usafi wa mazingira ni za kila mmoja kwani inapotokea faida au athari za mabadiliko ya tabianchi zinawakuta wananchi wote. Kwa niaba ya Mabalozi wenzangu wa mazingira, tunatoa hamasa ya upandaji miti na usafi wa mazingira na kuhamasisha vijana kuendelea kujitolea kuitunza miti iliyopandwa kwa kuimwagilia maji lengo likiwa ni kuhakikisha miti iliyopandwa inakua kama ilivyotarajiwa", amesema Bw. Mushi.