Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Madarasa 29 ya Mil. 580 Kukamilika Dodoma Wiki Ijayo
Nov 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha Shilingi 580,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 29 ya shule za sekondari kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa nafasi na katika mazingira bora.

Shukrani hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipofanya ziara ya kawaida kutembelea shule ya sekondari Miyuji iliyopo jijini hapa.

Mafuru alisema “kwa mara nyingine tena tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa hili alilotufanyia Jiji la Dodoma, ametufanyia mara ya pili mfululizo kwa elimu ya sekondari. Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma hatutarajii watoto watakaofaulu darasa la saba kupata shida kujiunga na kidato cha kwanza watakuta madarasa yote yapo kamili. Kwa hiyo, mwezi Januari ni kuingia darasani na kusoma”.

“Nimezunguka baadhi ya shule kukagua hali ya ujenzi wa madarasa unavyoendelea. Nanyi mmejionea katika shule hii ya sekondari Miyuji wapo kwenye ‘roofing stage’. Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilitupatia muda wa mwisho kumaliza ujenzi wa madarasa haya tarehe 15 Disemba, 2022 kuwa tumekamilisha ujenzi wa madarasa yote 29. “Sisi tuliporudi ofisini tukasema hebu tutengeneze programu yetu ya ndani ili tuwe na muda wa kutosha kufanya marekebisho pale yatakapohitajika. Nimeongea na Mwalimu Maige na mafundi hapa tunakabidhiwa madarasa haya tarehe 15 Novemba, 2022” alisema Mafuru.

Akiongelea kasi ya ujenzi huo kwa shule nyingine zinazotekeleza ujenzi wa madarasa hayo alisema kuwa inaenda vizuri. “Nimeongea na Afisa Elimu Sekondari, Madam Upendo Rweyemamu na kunihakikishia kuwa maeneo yote kasi inalingana. Hivyo, tupo asilimia 90 ya ujenzi kwenye madarasa haya. Bahati nzuri Afisa Elimu alishatoa maelekezo kwamba wakati tunaendelea na ujenzi huu waanze kutengeneza meza na viti. Nimekuta tayari shule ya sekondari Miyuji wameshaanza na kuandaa viti na meza 100 na tarehe 15 tunakabidhiwa madarasa, viti na meza” alisema Mafuru.

Akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Miyuji, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Greyson Maige alisema kuwa shule yake ilipokea Shilingi 40,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja.

“Baada ya kupokea fedha hizo tulipokea maelekezo toka Ofisi ya Mkuregenzi juu ya matumizi ya ‘force account’. Tuliunda kamati tatu. Kamati ya ujenzi, manunuzi na mapokezi ya vifaa. Baada ya hapo tukafanya taratibu za kumpata fundi, tukafanya taratibu za kupata wazabuni walio bora. Mpaka sasa mradi umefikia hatua nzuri. Ofisi ya Mkurugenzi imetusaidia sana na kamati za shule zimetusaidia sana. Wanakamati wamefanya kazi kwa weledi bila kuchoka”, alisema Maige.

Akiongelea faida za mradi huo, alizitaja kuwa ni wanafunzi kuwa na madarasa bora kwa ajili ya kujifunzia na kupunguza mrundikano madarasani na walimu kuweza kufundisha vizuri na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Awali akitoa maelezo ya utangulizi kwa Mkurugenzi wa Jiji, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa jiji hilo lilipokea fedha Shilingi 580,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 29, na shule ya sekondari Miyuji ni moja ya shule zinazotekeleza ujenzi wa madarasa hayo ikiwa inajenga madarasa mawili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi