Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Madaktari Nchini Watakiwa Kuzingatia Uadilifu, Umakini, Kujitolea na Uzalendo wakati Wakihudumia Wananchi
Oct 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Madaktari nchini wametakiwa kuzingatia uadilifu, umakini, kujitolea na uzalendo wakati wakitekeleza majukumu yao wanapowahudumia wananchi.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa  Dodoma, Dkt. Fatma Mganga mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa Madaktari na watoa huduma za afya kutoka Mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida na Dodoma ya namna ya kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa wafanyakazi walioumia au kuugua kutokana na kazi.

“Mafunzo mmeshapata, ninachofanya ni kukazia kwenye suala la integrity (uadilifu), seriousness (umakini), commitment (kujitolea) na uzalendo, tunakwenda kufanya tathmini za watu walioumia kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, anayestahili fidia ndogo apewe fidia ndogo kulingana na ajali aliyopata na anayepata fidia kubwa apewe fidia kubwa na usiangalie mtu aliyefika mbele yako ni wa aina gani.” Alifafanua Dkt. Mganga.

Alisema ni wajibu wa Daktari kumdodosa mteja wake (mgonjwa) kwani itamsaidia kujua historia yake na na hivyo kumuwezesha kujua kama tatizo lililomleta lina uhusiano na kazi aliyokuwa akifanya au ni matatizo yaliyo nje ya kazi anayoifanya.

“Kama Daktari hauko makini na kuwa mdodosaji (inquisitive) na ukienda juu juu mteja (mgonjwa) atakudanganya, lazima ujue zaidi ya kile unachokiona machoni, hii itakusaidia kutoa ripoti sahihi na hivyo kuuwezesha Mfuko kutoa Fidia Stahiki.” Amesisitiza Dkt. Mganga, ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar alisema mafunzo hayo yalihusisha madaktari 85 na hivyo kufanya idadi ya Madaktari waliopatiwa mafunzo kama hayo kufikia 1,386 nchi nzima.

Alisema Mfuko umeweka mkazo mkubwa wa kutoa mafunzo kwa madaktari kote nchini ili kuwajengea uwezo wa kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa wafanyakazi walioumia au kuugua kutokana na kazi wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri kwa mujibu wa mkataba.

“Wenzetu hawa madaktari ni daraja muhimu baina ya Mfuko na wafanyakazi, elimu hii tuliyowapatia itawasaidia wafanyakazi wote watakaopita kwenye mikono yao kupata matibabu stakihi lakini pia kupata fidia stahiki kwa mujibu wa sharia ya fidia kwa wafanyakazi.” Alibainisha Dkt. Omar.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Dkt.Nasibu Msuya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kitete mkoani Tabora aliushukuru Mfuko kwa mafunzo hayo kwani yamewapa uelewa mkubwa wa jinsi mfanyakazi anavyoweza kulipwa fidia pindi anapopata matatizo awapo kazini.

“Kazi yetu kubwa ni kufanya tathmini ya ulemavu yaani Impairment assessment (kiwango cha madhara aliyopata mfanyakazi) na disability (ulemavu) inafanywa na wataalamu wa WCF wenyewe.” Alisema.

Alisema mafunzo hayo yamewawezesha kujua taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa mfanyakazi anayeumia au kuugua kitokana na kazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi