Na Mwandishi Wetu
BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Richard Mayongela kwa kuthibitishwa rasmi katika nafasi hiyo.
Awali Bw. Mayongela alikuwa akikaimu nafasi hiyo kwa takribani miezi 11 iliyopita.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa MAB, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema kwa niaba ya bodi nzima amesema "Nimepokea taarifa rasmi ya kuthibitishwa kwako kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania. Ninakupongeza."
Mhandisi Prof. Lema amesema kutokana na wadhifa huo, anatumaini makubwa Mkurugenzi huyo ataendelea kuiongoza Mamlaka hiyo kwa utendaji makini na kwa weledi wa hali ya juu unaozingatia ufanisi na uadilifu usio na shaka yoyote.
Pia amemtaka Bw. Mayongela kujenga timu yenye nguvu kwenye Mamlaka
itakayoongozwa kwa misingi ya dira sahihi na mwelekeo mmoja kwa
wote, unaoheshimu na kuzitumia fani za kila mtumishi wa Mamlaka
ipasavyo kwa manufaa mapana ya Taifa.
"Mungu akuzidishie hekima katika majukumu yako," amesema Mhandisi Prof. Lema.
Uthibitisho huo uliwasilishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issac Kamwelwe na kusomwa katika mkutano wa Mameneja wa Viwanja vya Ndege Tanzania uliofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias.
Halikadhalika, Bw. Mayongela baada ya uthibitisho huo rasmi aliwashukuru
Watumishi wote wa Mamlaka na kusema hatua hiyo imechangiwa na juhudi za pamoja na ushirikiano kwa kipindi chote cha takribani miezi 11 alichokuwa akikaimu nafasi hiyo.
"Bila nyie nisingeweza kufanya kitu chochote, na hali kadhalika bila ushirikiano wenu peke yangu nisingeweza," amesema Bw. Mayongela.
Hatahivyo amewasisitizia Watumishi wenzake kuchapa kazi kwa weledi, bidii, maarifa na uzalendo mkubwa usioweza kutiliwa mashaka ya aina yoyote kwa kuwahudumia Wadau na Watanzania wote kwa ujumla ili kuleta tija kubwa kwa taifa.