Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maandalizi ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Njombe Yapamba Moto
Feb 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na: Mwandishi Wetu – Njombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amepongeza Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa hatua nzuri waliyofikia kuelekea katika uzinduzi wa tukio hilo muhimu linalotarajiwa kufanyika Aprili 2, 2022 Mkoani Njombe.  

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye kamati hiyo, Waziri Ndalichako alieleza kuridhishwa na hatua za awali za maandalizi na kuipongeza kamati ya Mkoa kwa kuendelea kusimamia na kuratibu vyema shughuli hiyo ya maandalizi.

“Kwa namna maandalizi haya yanavyoendelea vizuri inadhihirisha kuwa tulifanya maamuzi sahihi kuteua Mkoa wa Njombe kuwa ni sehemu ambayo Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa,”

“Hongereni kwa maandalizi ambayo mmefanya mpaka sasa na niwapongeze kwa kuonyesha utayari wa kuhakikisha shughuli hii ya kitaifa inafana, maana maandalizi mazuri yataleta heshima kwa Mkoa huu, hivyo mzingatie masuala yote ya msingi yatakayofanya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Njombe una kuwa wa kihistoria,” alisema Waziri Ndalichako.

Aliongeza kuwa, kila mwaka Mwenge wa Uhuru hukimbizwa katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini ikiwemo Bara na Visiwani.

Waziri Ndalichako alifafanua kuwa Serikali imepanga kufanya Sensa ya Wat una Makazi mwezi Agosti 2022, hivyo kauli mbiu ya Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2022 ni; Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo; Shiriki Kuhesabiwa, Tuyafikie Maendeleo ya Taifa. 

Sambamba na hayo Mheshimiwa Ndalichako aliwasihi wajumbe wa Kamati hiyo ya Mkoa kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao katika shughuli hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani humo.

Pia, Waziri Ndalichako alipokeza Mkoa kwa namna umekuwa ukishirikisha wadau ili waweze kujitokeza na kuchangia ufanikishaji wa shughuli hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru. 

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mhandisi Marwa Rubirya alisema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema na maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru na aliahidi kusimamia shughuli zote za maandalizi kwa ufanisi na kukamilisha ndani ya muda uliopangwa.

“Nikuhakikishie uteuzi huu tutautendea haki na tutawezesha wananchi wa Mkoa wa Njombe wanashiriki katika tukio hilo muhimu na kutumia fursa hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kujitangaza kama Mkoa,” alisisitiza Mhe. Rubirya

Katika ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alitembelea Uwanja wa Sabasaba ambapo uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kufanyika, pia aliwatembelea vijana wa Halaiki katika Shule ya Sekondari Mpechi Mkoani Njombe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi