Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maandalizi ya Uzinduzi wa Matokeo ya Sensa Wakamilika
Oct 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho


• Rais Samia Mgeni Rasmi


Na Mwandishi wetu- Dodoma

Maandalizi ya Sherehe ya uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 yamekamilika na yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali pamoja na Marais Wastaafu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na wadau wengine wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, George Simbachawene amesema kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo utakaofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine. Hivyo, uzinduzi huu ni tukio moja muhimu ndiyo maana Serikali imeamua kuhakikisha kuna uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria”. Ameeleza Simbachawene.

Ameongeza kuwa mbali na uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan atazindua Mwongozo Maalum wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

”Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi”. Amesisitiza Simbachawene.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamza Hassan Juma amesema kuwa Serikali inawashukuru watanzania kwa kujitokeza kushiriki katika zoezi la Sensa.

Aidha, amewataka Watanzania wote kujitokeza kushiriki katika uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi na pia amevishikuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri vinayoendelea kufanya katika kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi