Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani ni ya Watu Wote - Ndalichako
Sep 20, 2023
Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani ni ya Watu Wote - Ndalichako
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani leo jijini Dodoma.
Na Adelina Johnbosco - MAELEZO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani yatakayofanyika kuanzia Septemba 25 hadi 30, 2023 jijini Mbeya ni kwa ajili ya watu wote na si watu wenye ulemavu wa kusikia pekee.

Amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo, 'Dunia Ambayo Popote Walipo Viziwi Wanaweza Kutumia Lugha ya Alama' ambapo amewata wananchi wote kujitokeza kushiriki maonesho hayo, kwani watapata elimu mbalimbali kuhusu masuala ya viziwi ili wajue jinsi ya kuwa msaada kwa watu wenye changamoto ya kutosikia au usikivu hafifu.

Maazimisho haya yanakuja ikiwa ni mwendelezo wa tangu Shirikisho la Viziwi Duniani (WFD) lilipozindua Siku ya Viziwi Duniani mwaka 1958 ili kuibua changamoto zinazowakumba viziwi na namna ya kuzikabili.

"Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika wiki ya Viziwi Duniani ili kutoa fursa kwa viziwi kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana na jamii inayowazunguka bila ya kuwepo vikwazo vyovyote ikiwepo vikwazo vya mawasiliano yao," amesema Ndalichako.

Aidha amesisitiza juu ya matumizi ya lugha ya alama ili kuwafanya viziwi kuelewa na  kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii kwani nao ni wananchi kama wengine.

Licha ya jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha kundi hili haliachwi nyuma ikiwemo kuwezesha uwepo wa kamusi ya kidijitali ya lugha ya alama, kusomesha na kuongeza wataalam wengi, kuweka vifaa vya kiafya kutambua tatizo kwa watoto wangali wadogo ili kuweza kukabiliana na tatizo, Waziri Ndalichako ametoa wito kwa taasisi na ofisi zote nchini kuwa na utaalam wa lugha ya alama kwenye sehemu zao za kutolea huduma.

"Serikali inasisitiza kuhakikisha kila taasisi inayotoa huduma kwa jamii inakuwa na mkalimani wa lugha ya alama sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wake kuwa na uelewa wa lugha ya alama ili watu wenye changamoto ya usikivu wapate haki yao ya kupata huduma stahiki," amesema Ndalichako

Kwa upande wake mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Mhe. Bw. Ernest Kimaya ameishukuru Serikali kwa kuwajali watu wenye ulemavu nchini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo kuwashirikisha kwenye fursa za kiuchumi.

Naye Adam Shaban, makamu mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) licha ya kutoa shukurani kwa Serikali jinsi inavyozidi kuwajali, lakini amewataka watu wote wenye ulemavu kushiriki maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ili kuendelea kujifunza na kupata uelewa zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi