Na Mbaraka Kambona,
Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) imewezeshwa vifaa vya kisasa katika maabara zake ambapo sasa wamekuwa na uwezo wa kutambua kwa haraka vimelea vya magonjwa ya mifugo ndani ya dakika 15 tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa inawachukua kati ya masaa 24 hadi 36.
Hayo yamefahamika leo Novemba 21, 2022, jijini Dar es Salaam wakati Mwakilishi kutoka Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim akimkabidhi Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga nyaraka za vifaa vya maabara ambavyo vimegharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania milioni 600.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Prof. Nonga alisema kuwa lengo la kuboresha maabara hizo ni kuzijengea uwezo hasa kwenye kubaini uwepo wa vimelea ambavyo vimepelekea matumizi makubwa ya dawa za antibayotiki kwenye mifugo hasa kuku.
“Kutokana na mazingira tuliyonayo Tanzania, uwepo wa vimelea haukwepeki kutokana na joto, mvua na hali ya unyevunyevu, na vimekuwa kikwazo kwenye uzalishaji na uzalianaji wa mifugo yetu, hivyo basi tunapokuwa na maabara zilizoboreshwa zaidi inakuwa ni rahisi kubaini aina ya kimelea na kuweza kujua aina ya dawa ambayo inaweza kutumika kutibu na kumsaidia mfugaji kufuga kwa tija na kuepukana na maradhi,”alisema Prof. Nonga
Aliongeza kwa kusema kuwa ili kuweza kupambana vyema na vimelea hivyo ni muhimu wadau wa mifugo wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya mifugo ili iweze kuwa na tija zaidi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Naye, Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Mifugo (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi alisema msaada huo walioupata kutoka kwa taasisi ya Fleming Fund kupitia taasisi ya American Society for Microbiology umesaidia kuwawezesha kufanya kazi zao kwa haraka zaidi.
“Kabla ya kupata vifaa hivi ilikuwa inatuchukua masaa zaidi ya 24 kutambua vimelea vya magonjwa ya mifugo lakini baada ya kupata msaada huu sasa tunaweza kutambua vimelea ndani ya dakika 15 tu,”alifafanua Dkt. Bitanyi
Aliongeza kuwa teknolojia hiyo ya kisasa waliyoipata inafanya maabara zao ziendane na teknolojia iliyopo duniani ambayo inawawezesha pia kutambua aina ya kimelea na ukoo wake.
Kwa upande wa Mwakilishi kutoka Taasisi ya American Society for Microbiology, Dkt. Wes Kim alisema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kupambana na vimelea vya magonjwa ya mifugo ili kuweka msingi mzuri wa afya ya mifugo na usalama wa chakula kwa jamii.
Aidha, taasisi hiyo pia iko mbioni kuzisaidia maabara nyingine zilizo chini ya TVLA ikiwemo ya Iringa ambayo hivi karibuni nayo itakabidhiwa vifaa kwa lengo hilohilo la kuboresha utendaji wa maabara hizo nchini.