Leseni Mpya 80 za Maduka ya kubadilishia fedha zatolewa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania baada ya waombaji kukidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 26, 2023 uliolenga kueleza utekelezaji wa Serikali.
" Utaratibu wa kutoa leseni za maduka ya kubadilishia fedha ulisitishwa kutokana na Changamoto mbalimbali, sasa Serikali imejiridhisha na utaratibu wa utoaji leseni hizo unaendelea ikiwa ni dhamira ya Serikali kukuza sekta ya fedha nchini", alisitiza Bw. Msigwa.
Akieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na upungufu wa dola amesema ni pamoja na kununua dhahabu kilo 400 kati ya Mei na Julai 2023.
" Dola Milioni 20 zimetolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa bei ya jumla kwa mabenki yetu hapa nchini", alisisitiza Bw. Msigwa.
Hatua nyingine ni pamoja na kusaidia wafanyabiasha kuongeza mauzo ya nje na pia kutafuta mikopo itakayosaidia kuongeza dola za Marekani hapa nchini.
Sanjari na hatua hizo zaidi ya Shilingi Bilioni 9 zilizokuwa zimezuiliwa zimerejeshwa kwa wamiliki wake.
Msemaji Mkuu wa Serikali amekuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa Wananchi kwa lengo la kuimarisha Mawasiliano ya Serikali na Wananchi wake.