Na: Agness Moshi - MAELEZO
Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa LAPF, umedhamiria kuwawezesha wafugaji hapa nchini, kwa kujenga machinjio ya kisasa Mkoani Morogoro ambayo itazalisha ngozi kwaajili ya Viwanda pamoja na kusindika nyama kwaajili ya kuuza nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa LAPF Bwana.Eliud Sanga wakati wa mahojiano maalum katika kipindi cha tunatekeleza kinachorushwa na Televisheni ya Taifa TBC Jumatatu hii.
Bw. Sanga alieleza kuwa machijio hayo ambayo yamekamilika kwa Zaidi ya asilimia 80, yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 kwa siku na yataongeza idadi ya ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro na vitongoji vyake.
Alieleza kuwa kuanzishwa kwa machinjio hayo ni katika kuongeza uwekezaji na kuunga mkono juhudi za Mh.Rais Dkt.John Pombe Magufuli za kujenga Tanzania yenye uchumi wa Viwanda.
“Bwana Sanga amesema kuwa ngozi zitakazopatikana kwenye machinjio hayo, zina uhakika wa soko kwa asilimia kubwa kwani kuna viwanda vinavyoshughulika na utengenezaji wa bidhaa za ngozi nchini na nje ya nchi vinavyohitaji malighafi hiyo”. Alisema Bw. Sanga.
Aidha Bwana Sanga ameongeza kwa kusema kuwa viwanda vya ngozi nchini vitafaidika kwa uwepo wa machinjio hayo kwani watakuwa na uhakika wa kupata ngozi zilizozalishwa katika viwango vya ubora unaokidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa LAPF itawekeza kwenye kuandaa wafugaji kwa kuwapa elimu ya jinsi ya kufuga ng’ombe kisasa pia kutambua aina na umri wa ng’ombe watakaohitajika katika machinjio hayo.
Mfuko wa pensheni wa serikali za Mitaa LAPF ni mfuko wa hifadhi ya jamii ulionzishwa na serikali ya kikoloni ya Tanganyika mwaka 1944 ukiwa na lengo la kuweka akiba wafanyakazi wa hali ya chini, ambapo uliendelea kubadilika kiutendaji hadi mwaka 2006 ambapo ulibadilisha mfumo wa uendeshaji na kuwa mfuko wa pensheni.
Mfuko huu kama ilivyo mifuko mingine ya hifadhi ya jamii pia umejikita katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uwekezaji kwenye vitega uchumi pamoja na ulipaji wa mafao kwa wanachama.