Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Serikali imesema kuondolewa kwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vya ujenzi kwa lengo la kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi kutawanufaisha wafanyabiashara wachache kuliko wananchi wa kawaida na kupunguza mapato ya Serikali.
Hayo yamesemwa Bungeni leo Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Godbless Lema juu ya Serikali kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi.
“Matumizi ya vifaa vya ujenzi ni mtambuka, ni vigumu kutambua kama mnunuzi atatumia kwa ujenzi wa makazi binafsi, biashara au miundombinu kama barabara” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza kuwa lengo la kutoza kodi ni kuiwezesha Serikali kuwa na mapato ya kutosha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma muhimu za kijamii kwa Wananchi wake.
“Uhai wa Taifa lolote ni kodi hakuna maendeleo yanayopatikana katika Taifa lolote bila kodi hivyo makusanyo ya kodi ndio yanasababisha Serikali kuweza kutoa huduma nyingi bure kwa wananchi wake”. Amefafanua Dkt. Kijaji.
Hata hivyo Dkt. Kijaji amesema kuwa nyumba zinazojengwa na kuuzwa na Shirika la Nyumba la Taifa ni mradi wa kibiashara na si huduma, pia wauzaji wa nyumba hapa nchini ni wengi hivyo kuondoa kodi ya VAT kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba la Taifa peke yake utakua ni ubaguzi kwa wauzaji wengine wa nyumba ikiwa na kuikosesha Serikali mapato kwa manufaa ya Taifa