Na Shamimu Nyaki - Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali inakusudia kurejesha Kombe la Muungano ili kukuza vipaji na kupata wachezaji watakaotumikia Timu ya Taifa.
Mhe. Gekul amesema hayo leo Septemba 13, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Suleiman Haroub Suleiman ( BLW) aliyeuliza Je, Ni vigezo gani vinatumika kuchagua wachezaji wa Timu ya Taifa ( Taifa Stars).
Akijibu swali hilo Mhe. Gekul amesema miongoni mwa vigezo ni mchezaji kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mchezaji awe anacheza Klabu ya Ligi za juu, na ufanisi mzuri kiuchezaji, nidhamu ya kiuchezaji na nidhamu ya kawaida pamoja na ufanisi mzuri kiuchezaji.
"TFF na ZFF zinashirikiana katika kutafuta wachezaji watakaotumikia Timu ya Taifa, namashirikisho hayo hushiriki kikamilifu katika Benchi la ufundi la kuchagua wachezaji hao" amesisitiza Mhe.Gekul.
Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Haroub Suleiman Haroub kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika kutoa wachezaji Mhe. Gekul amesema mashirikisho ya Mpira wa Miguu TFF na ZFF yanashirikiana vyema katika michezo na yataendelea kufanya hivyo sio tu kufanikisha matokeo mazuri ya timu ya Taifa, lakini pia kudumisha Muungano adhimu uliopo.
Mhe Gekul wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Abbasi Tarimba Kuhusu Idadi kubwa ya wachezaji wa nje katika Klabu Hali inayozorotesha upatikanaji wa wachezaji wa timu ya Taifa, amesema Serikali imeishauri TFF kuzingatia Idadi ya wachezaji wa ndani katika Klabu ili waoneshe uwezo walionao na hatimaye kupata timu bora ya taifa.