Na Lilian Lundo - MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka Wakulima kuendelea kulima na kufuata utaalam kwani kilimo kinalipa na ni biashara.
Msigwa amesema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) leo Julai 08, 2022 Jijini Dar es Salaam.
“Kwenye kilimo ndipo Watanzania tunapategemea, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanategemea kilimo na wameajiriwa kwenye sekta ya kilimo, chakula chetu Tanzania tunategemea kwenye sekta ya kilimo,”alifafanua Msigwa.
Aliendelea kusema kuwa, kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo serikali imeongeza bajeti kwenye sekta hiyo kutoka shilingi bilioni 294 kwa mwaka wa fedha 2021/2022mpaka shilingi Trilioni moja kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili wakulima walime kwa ubora, wazalishe kwa kutumia mbegu bora na kulima kilimo cha umwagiliaji na sio chakutegemea mvua peke yake.
Aidha, amewapongeza wizara ya kilimo na taasisi zake kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuhakikishwa wakulima wanapata huduma zote zinazotakiwa kama vile kupata mbegu bora zenye mazao mengi. Pia amewataka wakulima kutumia matokeo ya utafiti unaofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutokana na wakulima wengi kulima kilimo cha mazoea kwa kutumia mbegu ambazo hazina tija na hazihimili magonjwa.
Kwa upande wake Mchumi wa Wizara ya Kilimo, Maria Mtui amesema kuwa kwa sasa Tanzania inasafirisha mazao ya chakula kama vile Mchele na Mahindi nje ya Tanzania na mazao hayo sasa yamekuwa moja ya mazao ya biashara na sio chakula peke yake kama ilivyokuwa ikichukuliwa kipindi cha nyuma.
“Mauzo ya mchele nje ya nchi yemeongezeka kutoka tani 184,521 zenye thamani ya shilingi 176.4 mwaka 2021 hadi tani 441,908 mwaka 2021 zenye thamani ya shilingi Bil. 476.8 mwaka 2021, mahindi kutoka tani 92,825 zenye thamani ya Shilingi Bil. 58 mwaka 2020 hadi tani 189,277 zenye thamani ya Shilingi Bil. 72.4 mwaka 2021,” alifafanua Maria.