Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kila la Heri Serengeti Girls: Naibu Waziri Gekul
Oct 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameitakia kila la heri Timu ya Wasichana chini ya miaka 17, (Serengeti Girls) katika mechi ya mwisho ya Kundi D dhidi ya Canada itakayochezwa Oktoba 18, Uwanja wa DY Patil Navi Mumbai majira ya Saa 2: 00 usiku saa za India sawa na  saa 12: 30 jioni  saa za Tanzania baada ya kuitembelea mazoezini jioni ya Oktoba 17, 2022.

Mhe. Gekul amewataka wachezaji hao kuingia uwanjani wakiwa na ari, kujiamini lakini pia kujua kuwa Watanzania wanahitaji kuona wanasonga mbele katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia.

"Tanzania tunahitaji ushindi ili tusonge mbele, mchezo mliocheza juzi na Ufaransa kaongezeni kasi maana Canada pia ni wazuri,  Rais Mhe. Samia na Waziri, Mhe. Mchengerwa wanaimani kubwa na nyie hivyo msiwaangushe,"amesisitiza Naibu Waziri Gekul.

Kwa upande wa Kocha, Bakari Shime amesema vijana wako vizuri kiakili na kimwili na wapo tayari kwa mchezo ambao utakua wa kujilinda na kushambulia.

Mechi hiyo ya mwisho kwa kundi D ni lazima Tanzania ishinde au ipate sare ya aina yoyote ili isonge mbele katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa  umri huo.

Katika kundi D  Tanzania ipo pamoja na Japan ambao wanaongoza kundi hilo na tayari wamefuzu hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi zote mbili walizocheza, huku nafasi ya pili imekamatwa na Tanzania, tatu Ufaransa na  nne ni Canada.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi