Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kigwangalla Atanzagaza Vita dhidi ya Majangili
Oct 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Jonas Kamaleki

Muda mfupi baada ya kula kiapo, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, ametoa onya kali kwa majingili nchini na kuwataka kuacha mara moja vitendo hivyo.

Dkt. Kigwangalla ametoa onyo hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuapishwa mawaziri na naibu mawaziri.

“Majangili waanze kukimbia wenyewe pale wanapowaona wanyama kwani tutawashughulikia ipasavyo na kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi viovu katika nchi yetu,” alisema Dkt. Kigwangalla.

Kuhusu utalii, Dkt. Kigwangalla amesema kuwa watalii wamekuwa wakiongezeka lakini si kwa kiwango cha kuridhisha hivyo Serikali itafanya juhudi za makusudi kutangaza vivutio vya utalii kwa njia za kisasa ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa ubunifu katika kujitangaza itabidi utumike ili kuhakikisha Tanzania inavutia watalii wengi kutoka nje hususan soko jipya la China na nchi nyingine ikiwemo Marekani na nchi za Ulaya.

Kwa kufanya hivyo pato la Taifa kutokana na utalii litaongezeka kuliko ilivyo sasa, alisema Kigwangalla.

Aidha, Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amesema atashirikiana na wizara nyingine kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji ili lipatikane suluhisho la kudumu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, amesema atahakikisha watumishi wa umma katika wizara yake wanafanya kazi kwa kujituma zaidi na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa mujibu wa Jafo, uadilifu, uwajibika na nidhamu ni mambo ambayo yatatiliwa mkazo katika wizara yake ili kuwa na utumishi wenye tija.

Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya kufanya kazi kwa mashindano ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo katika sehemu husika na kuchochea ukuaji wa uchumi hasa wa viwanda.

“Wakuu wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri muwe vinara katika utendaji wenu mkiwasimamia walioko chini yenu kwa weledi ili muweze kwenda na spidi ya Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Jafo.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akizungumza baada ya kuapishwa amesema atahakikisha sekta ya habari inapewa kipaumbele kwani habari ni jambo muhimu katika suala zima la mawasiliano.

Mhe. Shinza atahakikisha weledi katika sekata ya habari unazidi kuimarishwa ilikuondoa upotoshwaji ambao umekuwa ukijitokeza katika baadhi ya vyombo habari.

Kuhusu upatikanaji wa habari kwa sehemu kubwa ya watanzania, Shonza amesema atajitahidi kufanya habari ziwafakie watanzania wengi Zaidi ili kujenga jamii yenye ufahamu wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yao.

Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha jumla ya Mawaziri nane na Manaibu Mawaziri 16 ambao wameanza kazi mara baada ya kuapishwa kwa kuhudhuria kikao cha Maalum cha Baraza la Mawaziri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi