Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kigoma Yazindua Mpango Kazi Kutokomeza Ukatili wa Wanawake na Watoto
Dec 22, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na WAMJW, Kigoma

Mkoa wa Kigoma umezindua Mpango kazi kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinatokomezwa na kuondoa nafasi ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo.

Akizindua Mpango kazi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Rashid Mchatta amesema atasimamia Halmashauri kuhakikisha zinatenga bajeti kutekeleza mkakati huo kwani ni wajibu wa kila mmoja kuweka juhudi na jamii kuwa na uelewa kuhusu madhara ya vitendo hivyo.

"Yote ambayo yameazimiwa katika Mpango huu yatatekelezwa na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kutokomeza vitendo hivyo. Ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake awajibike baada ya kutoka hapa na tutakuwa tumewatendea haki wanawake na watoto. Suala la lishe na hili la ukatili wa watoto na wanawake tutayatilia mkazo", alisema Mchatta.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka ya Afya, Mwajuma Magwiza amesema Mpango kazi huo utaendeleza kwa kasi Kampeni hiyo ya Twende pamoja ukatili sasa basi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

"Suala hili sio la kuiachia Serikali ila wanajamii na wadau, sote kwa pamoja tuunge mkono juhudi hizi kwa kuweka bajeti zetu ambazo zote zitaelekeza nguvu katika kupambana na ukatili uliopo Mkoani Kigoma na Tanzania nzima" alisema Magwiza.

Aidha, Magwiza amehimiza Jamii ishirikishwe katika utekelezaji wa mpango huu na kupata taarifa katika kila hatua inayofikiwa.

Akiwasilisha Mpango kazi huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Grace Mwangwa ameikumbusha jamii kutekeleza wajibu wao kulingana na nafasi zao na kusema kuwa Mpango umejumuisha masuala mbalimbali yaliyoainishwa na Wadau katika kongamano lililofanyika awali.

Grace amesisitiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake kwenye Mamlaka ili hatua zichukuliwe kwa wanaofanya vitendo hivyo.

"Ukatili mwingi unaanzia ndani ya familia, kwa sababu vitendo vinapotokea wanaamua kuyamaliza nyumbani hali inayopelekea ukatili kuongezeka kwani wanaofanya vitendo hivyo wanakuwa hawajachukuliwa hatua", amesema Grace.

Kwa upande wake mmoja wa viongozi wa dini aliyeshiriki katika uzinduzi huo, Shekh Rashid Haruna Hamis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya MTAKUWWA katika Kata ya Gungu, Kigoma Ujiji amesema kuwa Serikali inafanya vema kushirikiana na Wadau wote katika kukemea vitendo vya ukatili, akitaja mmomonyoko wa maadili ni chanzo kikubwa kusababisha vitendo hivyo.

Baadhi ya wananchi na Wadau walioshiriki kuandaa Mpango kazi huo baada ya majadiliano ya kina, akiwemo Beatrice Mtesigwa na Gervas Lwako wamesema mitandao ya kijamii ni changamoto kwa kizazi cha sasa na kuomba Mamlaka zinazohusika kuhakikisha kesi za vitendo hivyo zinafanyiwa kazi haraka. 

Mpango kazi huo umeandaliwa kwa pamoja na wadau mbalimbali wa Mkoa huo walioshiriki kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kujadili namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili mkoani hapo na kukubaliana Kaulimbiu ya Mpango huo ni Twende Pamoja, Ukatili Kigoma sasa basi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi