Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha Amour amemtaka Mkandarasi anayejenga kiwanja cha Ndege cha Iringa kuhakikisha anafanya kazi yenye ubora, viwango na kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa.
Katibu Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati alipokuwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi na upanuzi wa kiwanja hicho na kuridhishwa na utekelezaji wa ujenzi huo unaotekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO Cooperation ltd.
"Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo lakini hakikisheni mnakamilisha kwa muda uliopangwa na kuzingatia viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba" amesema Balozi Aisha.
Balozi Aisha ameridhishwa kuona kuwa ujenzi huo unafuata mpango wa ramani za kiwanja hicho (master plan) kama ilivyoainishwa kwenye mchoro.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Iringa, Mhandisi Daniel Kindole alieleza kuwa ujenzi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kutua na kuruka ndege (runway), njia ya mchepuo (taxway) na maegesho ya Ndege (Apron), jengo la zimamoto na jengo la nishati ya umeme.
Aliongeza kuwa kazi inaendelea vyema na mpaka sasa imefika asilimia 47.93 ya utekelezaji wake.