Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire amewataka Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Sekta hiyo kuhakikisha zinasimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chini ya taasisi zao zinakamilika kwa wakati na kwa viwango.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la utiaji saini mikataba ya utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 baina yake na Wakuu wa taasisi, Migire amesema ufuatiliaji na usimamizi utapunguza ucheleweshaji hasa kwenye kukamilika kwani changamoto zitakazobainika wakati wa utekelezaji zitapatiwa ufumbuzi mapema.
“Wataalam wapo kwenye kaguzi kila siku, lakini utashangaa viongozi wakuu wakikagua miradi ndio wanabaini changamoto zilizopo, nendeni mkawatumie wataalam hao vizuri na kuwepo na ratiba maalum zinazotambulika za ukaguzi ili mbaini changamoto mapema na kuzitafutia ufumbuzi mapema pia”, amesema Katibu Mkuu Migire.
Aidha, Katibu Mkuu Migire amesisitiza pia umuhimu wa nidhamu katika matumizi ya fedha ambapo amesema ni jukumu la Wakuu wa Taasisi kuhakikisha fedha zinatumika vizuri kwa kuweka vielelezo sahihi baada ya matumizi ili kupunguza hoja ambazo zimekuwa zikiibuliwa kila mwaka na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ufuatiliaji na Tathmini Sekta ya Uchukuzi, Bi Devota Gabriel amesema tathmini iliyofanyika kwa mwaka 2022/23 imeonyesha taasisi zimefanya vizuri kwenye usimamizi wa miradi na mafunzo kwa watumishi hali inayoongeza morali za watumishi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), Bi. Christina Mwakatobe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka vigezo kwa Wakuu wa Taasisi kwani vinawafanya kujitathmini katika utendaji kwa kila hatua ya utendaji.
Zoezi la utiaji saini kwenye utendaji limefanyika kati ya Katibu Mkuu na Wakuu wa taasisi zaidi ya 11 zinazosimamiwa na Sekta ya Uchukuzi.