Na. Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, ameuagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuweka mikakati mahususi ya kiutendaji itakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara na kukuza ajira nchini.
Mtendaji Mkuu huyo wa Wizara ametoa agizo hilo alipokuwa akiwahutubia watumishi wa OSHA katika kikao chao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Shitindi alifafanua kwamba mikakati hiyo inapaswa kujikita katika kuimarisha mifumo ya kiutendaji itakayolenga katika kuboresha huduma zitolewazo kwa wateja na taasisi hiyo ya umma ili kuwaondolea usumbufu watu mbali mbali wanaofanya shughuli mbali mbali za kiuchumi hapa nchini.
“Wakati mwingine tunashindwa kujipanga vizuri katika utekelezaji wa kazi zetu na hivyo kuwasababishia usumbufu mkubwa wateja. Kwa mfano unakuta mkaguzi mmoja wa Usalama na Afya mahali pa kazi anapita katika eneo fulani la kazi asubuhi na mwingine anakuja katika eneo hilo hilo mchana wakati watu hawa wangeweza kufika katika eneo la kazi kwa pamoja na kukamilisha kazi zao za kaguzi kwa wakati mmoja,” alisema Shitindi.
Aidha Katibu Mkuu huyo aliwaasa watumishi hao kufanya kazi zao za kila siku kwa kuzingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kujiepusha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa.
“Maadili ya utumishi wa umma yanajumuisha mambo mengi ikiwemo mavazi stahiki, matumizi ya lugha nzuri wakati wa kuwasiliana na wateja na pia heshima baina ya watumishi na viongozi wao na miongoni mwa watumishi wenyewe,” alisema Shitindi.
Vikao vya baraza la wafanyakazi wa OSHA ambavyo hufanyika kwa mwaka mara mbili vina lengo la kutoa fursa kwa wafanyakazi kujadiliana mambo mbali mbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuleta ufanisi zaidi.