Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa ameikabidhi timu ya Twiga Stars kitita cha shilingi milioni 10 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia ushindi waliopata dhidi ya timu ya Ivory Coast.
Akikabidhi kiasi hicho cha fedha, Katibu Mkuu, Bw. Msigwa amesema wachezaji hao wanafanya kazi kubwa ya kuiwakilisha nchi kimataifa na Serikali ipo pamoja nao kwa kuwa wanaitangaza na kuipigania nchi yao.
“Mnapokuwa uwanjani katika mechi za kimataifa mnakuwa mmebeba matumaini ya Watanzania, katika mechi zote mlizocheza tumeona dhamira mliyonayo kwa nchi yenu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapongeza sana, anafurahi sana anapowaona mnacheza uwanjani, anafurahi sana mnapopata matokeo mazuri katika mechi zetu”, Katibu Mkuu Bw. Msigwa.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alisema amefurahi kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Mama Samia kuhamasisha vijana hao kujituma zaidi kupambania nchi yao lakini kubwa kwa vijana hao ni pale kuona Rais anatambua mchango wao.
“Fedha ni sehemu kubwa ya hamasa, kitendo cha Rais Samia kuwafuatilia vijana wetu na kutambua timu hiyo inacheza ni faraja kubwa kwao na imekuwa chachu ya kujituma wakiamini kuwa Mama yupo pamoja nao,” amesema Shime.
Naye Nahodha wa Twiga Stars, Joyce Lema amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuzidi kuwapa hamasa na kumuahidi kutomuangusha katika mashindano yote yaliyopo mbele yao.
“Kwa hamasa hii inaonyesha kuwa kuna kitu kimeongeza katika soka na wanawake, tunatamani siku moja viongozi kuendelea kujitokeza kwa wingi kusapoti soka la wanawake kama ilivyo kwa wanaume”, amesema Joyce.