Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka watendaji wa ofisi yake kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa malengo yanayopimika ili kuiwezesha serikali kufikia malengo na kuwahudumia wananchi.
Mhandisi Luhemeja ameyasema hayo Septemba 5, 2023 mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Prof. Jamal Katundu ambae amehamishiwa Wizara ya Maji.
Ameongeza kuwa, kazi ya kuhudumia wananchi haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi hawatashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kama timu huku wakizingatia weledi, uzalendo na ubunifu kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha, ameahidi kushirikiana na menejimenti na watumishi katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya ofisi hiyo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Prof. Jamal Katundu ameishukuru Menejimenti na Watumishi kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo ambao ulimwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.