Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Katazo la Uagizaji Vifaa Vya Umeme Nje ya Nchi Laongeza Idadi ya Viwanda Nchini
Oct 24, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_37318" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akitoa taarifa ya utangulizi kuhusu hali ya upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Awamu ya Tatu wa usambazaji umeme vijijini kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.[/caption]

Na: Teresia Mhagama, Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amesema kuwa katazo la Serikali la kuagiza nje ya nchi vifaa vya kujengea miundombinu ya usambazaji umeme kama transfoma, nyaya, nguzo na mita za umeme, limeongeza idadi ya viwanda nchini na kupelekea vifaa hivyo kupatikana kwa wingi na ndani ya muda.

Ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya utangulizi kuhusu hali ya upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Awamu ya Tatu wa usambazaji umeme vijijini kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“ Kuanzia mwaka 2016, hususan baada ya msisitizo wa Serikali kuwa vifaa vya kujengea miundombinu ya umeme vizalishwe hapa nchini, ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa nyaya umeongezeka kutoka kiwanda kimoja hadi vitano,” alisema Dkt Kalemani.

Ameongeza kuwa, kabla ya mwaka 2016 kulikuwa na viwanda vinne tu vya uzalishaji nguzo za umeme lakini baada ya katazo la Serikali, viwanda hivyo vimeongezeka na kufikia Tisa.

Aidha, amesema kuwa viwanda vya uzalishaji transfoma navyo vimeongezeka kwani kabla ya mwaka 2016 kulikuwa na kiwanda kimoja tu lakini hadi kufikia mwezi Septemba 2018 vimeongezeka viwanda viwili na kufanya idadi ya viwanda hivyo kuwa vitatu.

[caption id="attachment_37320" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Ufundi na Huduma kutoka REA, Bengiel Msofe, akitoa taarifa ya kuhusu hali ya upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Awamu ya Tatu wa usambazaji umeme vijijini kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.[/caption]

Kuhusu mita za Luku, amesema kuwa kabla ya mwaka 2016 hakukuwa na kiwanda kinachozalisha mita hizo lakini lakini hadi sasa kuna viwanda viwili vinavyozalisha mita.

“ Uwepo wa viwanda hivi nchini, si tu unatoa uhakika wa upatikanaji wa vifaa na unafuu wa bei, lakini pia vinaongeza ajira kwa wananchi wetu na kulipa kodi serikalini,” aliongeza Dkt Kalemani.

Ameeleza kuwa, uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini, kwa kiasi kikubwa umetatua changamoto ya upatikanaji wa vifaa ndani ya muda muafaka kwani viwanda hivyo vinazalisha vifaa vingi zaidi ya mahitaji ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema kuwa, viwanda vya nyaya vinazalisha nyaya zenye urefu wa kilomita 196,435 kwa mwaka za ukubwa mbalimbali huku mahitaji ya REA na TANESCO yakiwa ni jumla ya kilomita 73,654 kwa mwaka.

“Viwanda vya nguzo pia vinakidhi mahitaji kwani  vinazalisha nguzo 1,750,000 hadi 1,800,000 kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji ya jumla ya nguzo 800,000 kwa miradi ya REA na TANESCO,” alisema Dkt Kalemani.

Aidha amesema kuwa kuwa jumla ya transfoma 21,600 zinazalishwa kwa mwaka huku mahitaji yakiwa ni transfoma 7,490 na kwamba viwanda vya ndani ya nchi, vinazalisha mita 1,456,000 kwa mwaka na mahitaji ni takriban mita 500,000.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi na Huduma kutoka REA, Bengiel Msofe amesema kuwa, Serikali inaweka mkazo pia vifaa vingine vya umeme kama vyuma na vikombe (hardwares and insulators) vizalishwe hapa nchini na kwa sasa inaendelea kupima ufanisi wa kuzalisha vifaa vinginevyo (accessories) hapa nchini.

Ameeleza kuwa, endapo Serikali itaona kuwa kuna ufanisi wa kuzalisha vifaa vivyo hapa nchini, itaacha kuagiza vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi