Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kampuni ya Techno Net Scientific Yakutwa na Kemikali Kinyume cha Sheria.
May 19, 2017

     

Na. Jacquiline Mrisho.

Kampuni ya Techno Net Scientific inayojishughulisha na uingizaji pamoja na uuzaji wa kemikali imekutwa na kemikali zilizoingizwa nchini kwa njia za udanganyifu kwa kutumia vibali vya bandia. Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampuni hiyo kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza bidhaa hiyo. Prof. Manyele amesema kampuni hiyo ilikuwa na usajili wa miaka miwili kuanzia April 30 mwaka 2014 hadi Aprili 30, 2016 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali kampuni hiyo ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti cha usajili kitakapopatikana. “Ingawa shughuli zake zilisitishwa lakini kampuni hiyo iliendelea kufanya kazi bila kuwa na cheti cha usajili hivyo ofisi yangu iliungana na Mamlaka ya Kudhibiti dawa za kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa kufanya ukaguzi wa pamoja ambapo kwa sasa tumewaachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi wao” amesema Prof Manyele. Amefafanua kuwa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182 na kanuni zake inatoa masharti kuwa kila mtu anayetaka kujihusisha na shughuli za kemikali kwa namna yoyote ni sharti awe amesajiliwa na kufanyiwa ukaguzi. Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara wote wa kemikali na umma kwa ujumla kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu na wanaovunja matakwa ya Sheria katika uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali ikiwemo kemikali bashirifu nchini. Prof. Manyele amewaomba wananchi kutoa taarifa na kuwafichua wafanyabiashara wa kemikali wanaokiuka matakwa ya Sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria ambazo zitapelekea wengine kuwa na matumizi salama ya kemikali na kuzuia madhara kwa watu na mazingira.        

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi