Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamishina Jenerali TAKUKURU Atoa Rai kwa Wananchi Ndani na Nje ya Nchi Kutojihusisha na Dawa za Kulevya
Dec 06, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa Za Kulevya, Gerald Kusaya ametoa wito kwa Watanzania na wasio Watanzania wenye nia au mawazo ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya kuondokana na mawazo hayo na kujikita katika biashara nyingine halali itakayoweza kumsaidia.

Kusaya ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam wakati akielezea mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

“Kama kuna mtu au kikundi cha watu wanajihusisha au wenye nia ovu ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja na kujihusisha na biashara nyingine zenye uhalali ambayo zitaweza kumsaidia kwani mamlaka na vyombo vingine vya usalama vimejipanga na hatutamuogopa mtu yeyote katika masuala haya ya mapambano” amefafanua Bw. Kusaya.

Aidha, amesema kuwa kwa yeyote mwenye taarifa mbalimbali za mtu au kikundi cha watu kujihusisha na madawa au biashara ya madawa ya kulevya kutoa taarifa kwa mamlaka na kubainisha kuwa taarifa hizo zitakuwa siri baina ya mtoa taarifa na mamlaka.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya uhuru katika Mmlaka hiyo, Kamshna Jenerali Kusaya anaeleza kuwa, toka kuanzishwa Mamlaka mwaka 2017 hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2021 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola Mamlaka ilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 45,784 wa dawa za kulevya, kilogramu 356,563.1 za dawa za kulevya pamoja na ekari 628.75 za mashamba ya bangi ziliteketezwa.

“Mchanganuo wa watuhumiwa na uzito wa dawa za kulevya zilizokamatwa ni kama ifuatavyo; Watuhumiwa 2,231 walikutwa na Heroin, 502 walikutwa na Cocaine, 37,743 walikutwa na Bangi, na 5,308 walikutwa na Mirungi; Aidha, Dawa za kulevya zilizokamatwa kwa uzito ni Kilogramu 1,125.41 za heroin, Kilogramu 26.67 za cocaine, Kilogramu 199,740 za bangi, Kilogramu 97,640 za mirungi, Kilogramu 57,600 za Kemikali Bashirifu, na Kilo 431.02 za Methamphetamine” amefafanua Bw. Kusaya.

Aidha amebainisha kuwa, jitihada za Serikali za kupambana na dawa za kulevya zimefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya nchini ambapo kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), nchi ya Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka Nchi zalishaji kwa zaidi ya asilimia 90.

Vilevile ameeleza kuwa, Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na taasisi nyingine zisizo za Kiserikali imefanikiwa kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini.

“Huduma hii, ilianza rasmi Nchini mwaka 2011 ambapo hadi 2016 kulikuwa na vituo vitatu tu nchini ambavyo vilihudumia waathirika 3,500, hivyo tangu kuanzishwa kwa Mamlaka, kumekuwa na ongezeko la vituo nane na hivyo kufanya jumla yake kuwa vituo kumi na moja (11) mpaka sasa vikihudumia zaidi ya waathirika 10,565 kila siku” anaongeza Bw. Kusaya.

Mbali na hayo Mamlaka imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake. Aidha, wenye matatizo yaliyosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya wapatao 169,269 walipatiwa huduma za tiba katika Vitengo vya afya ya akili Nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi