Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Pamoja ya Wataalam wa Mipaka ya Tanzania na Kenya Yakagua Mpaka
Apr 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM SERENGETI

Timu ya Wataalamu wa Mipaka kati ya Tanzania na Kenya imetembelea na kujionea kazi ya uimarishaji mipaka wa Kimataifa wa nchi hizo iliyofanywa kwa lengo la kukagua na kushauri namna bora ya kuendelea na kazi zinazofuata.

Ukaguzi wa mipaka hiyo ulifanyika tarehe 12 Aprili 2022 na ni sehemu ya kikao cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wa nchi hizo kilichotangulia awali kwa ajili ya kupokea  mawasilisho ya kazi iliyofanyika sambamba na kutoa muongozo wa namna bora ya kutekeleza kazi iliyobaki.

Wataalam hao wakioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor pamoja na Juster Nkoroi Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO) walitembelea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kirongwe wilayani Rorya kwa upande wa Tanzania na Muhuru Bay katika Kaunti ya Migori nchini Kenya pamoja na mpaka wa nchi hizo eneo la Serengeti/Masai Mara ili kukagua kazi ya uwandani.

Timu ya wataalamu wa mipaka kutoka nchi za Tanzania na Kenya tayari imekamilisha uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo kipande cha Kilomita 83 kutoka hifadhi ya Serengeti/ Masai Mara hadi Ziwa Natron, awamu ya pili ya kipande cha kilomita 110 uimarishaji wake utaendelea baada ya kukamilika kuandaliwa mpango kazi.

Wakati wa ufunguzi wa kikao cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wa nchi hizo mbili, Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mangwela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, aliwaambia washiriki kuwa, uimarishaji mipaka ulenge kuimarisha mahusiano pamoja na kujadili changamoto za maeneo ya mipakani.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Balozi Joseph Vungo alishauri wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kuhakikisha wanajadili na kuzitolea maamuzi changamoto kwa amani hasa wakizingatia nchi ya Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri.

Mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la nchi kavu una ukubwa wa Kilomita 758 na uimarishaji wake utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijotokeza kutoka kwa wananchi wanaofanya shughuli maeneo ya mipakani katika nchi hizo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi