Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Mawaziri Wizara za Kisekta Yaanza Ziara Mikoa 14 Kutatua Migogoro ya Matumizi ya Ardhi
Oct 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM RUKWA

Mawaziri wa Wizara za Kisekta, wameanza ziara ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

Ziara ya Mawaziri hao imeanza leo tarehe 11 Oktoba 2022 katika Mkoa wa Rukwa na itaendelea katika Mkoa wa Katavi tarehe 12 Oktoba 2022 kabla ya kuelekea Kigoma Oktoba 13, 2022.

Katika mikoa hiyo mitatu ya mwanzo, Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta itaoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Mashimba Ndaki.

Mikoa mingine itakayotembelewa na Kamati hiyo itakayohitimisha ziara yake Oktoba 28, 2022 mkoani Dar es Salaam ni pamoja na Kagera, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Wakati wa ziara yake, Kamati itakutana na Sekreterieti za Mikoa na Wilaya na kutoa mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 pamoja  na kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro.

Baadhi ya mapendekezo ya kamati kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi, kuhakiki pamoja na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji vya mita 60 na kufutwa kwa mashamba yasiyoendelezwa.

Tayari timu za wataalamu kutoka wizara za kisekta ziko uwanjani katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo kuhakikisha Kamati ya Mawaziri inafanya kazi yake kwa ufanisi

Mawaziri wanaoshiriki ziara hiyo mbali na Mhe. Dkt. Mashimba Ndaki ni Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Joseph Silinde, Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Mary Masanja, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Khamis Hamza Chillo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi