Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, leo tarehe 11 Oktoba, 2022 imefanya ziara ya kukagua miundombinu ya kupokea na kuhifadhi mafuta kwenye Bandari ya Mtwara na kupongeza Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo inafanya nchi kuwa na uhakika wa uwepo wa mafuta.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la kupokea mafuta katika Bandari ya Mtwara, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo ameelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri zinazofanywa na PBPA kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania, Wakala wa Vipimo na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, katika zoezi zima la kuagiza na kupokea mafuta na kuiepusha nchi na changamoto ya kukosa mafuta kama baadhi ya nchi zilizopatwa na changamoto hiyo kufuatia vita ya Urusi na Ukraine.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ameeleza kuwa Kamati hiyo itaishauri Serikali kuhusu masuala ya ununuzi wa mafuta kwa wafanyabiashara wa mafuta wa Mtwara kwa lengo la kuifanya Mtwara kuwa kivutio cha uwekezaji kwenye miundombinu ya hiyo itakayochochea kukua kwa uchumi wa Mikoa ya Kusini na kuongeza biashara kwa nchi zinazoweza kupata huduma kupitia bandari ya Mtwara Amezitaja nchi hizo kuwa ni Msumbiji, Comorro na Malawi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta Kwa Pamoja, Erasto Mulokozi ameeleza kuwa, hali ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa sasa ni nzuri.
Amesema, kwa sasa kuna upanuzi umefanyika katika miundombinu ya kuhifadhi mafuta mjini Mtwara ambapo kampuni ya GM imekamilisha ujenzi wa tenki la mafuta lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 na hivyo kufanya jumla ya hifadhi ya mafuta katika Bandari ya Mtwara kufikia lita milioni 35.
Amesema uwekezaji huo utaongeza uwezekano wa kuleta meli yenye mafuta mengi zaidi ikilinganishwa na sasa na hivyo kuleta unafuu wa bei za mafuta kwa mlaji wa mwisho.