Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeishauri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira kupanua wigo wa fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi.
Akizungumza leo Oktoba 17, 2023 katika kikao cha kamati hiyo cha kupokea na kujadili utendaji kazi wa kitengo hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq, amesema pamoja na juhudi za serikali kufungua fursa za ajira kuna umuhimu wa kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za ajira nje ya nchi.
Pia, ameshauri kufanyika kampeni maalum ya kukutana na wakala binafsi wa ajira ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Naye, Waziri wa Nchi wa Ofisi, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameahidi kufanyia kazi maoni ya kamati huku akimshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ambazo amezichukua za kukuza uwekezaji nchini na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas Katambi, amewahimiza Watanzania wanaotaka kufanya kazi nje ya nchi kufuata utaratibu unaotambulika na serikali ili iwe rahisi kusaidiwa wanapopata changamoto.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kitengo hicho kimetokana na kufutwa kwa Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) na majukumu yake kuunganishwa chini ya Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi.
Akitoa taarifa kwa kamati, Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Joseph Nganga amesema miongoni mwa majukumu ya kitengo ni kuwajengea uwezo wahitimu kushindana kwenye soko la ajira, kujenga mtazamo chanya kuhusu kazi na kukuza maadili yanayohitajika na waajiri.