Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko la Kariakoo unaotarajia kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu hatua itakayowezesha wafanyabiashara kurejea.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lazaro Nyamoga mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko la Kariakoo (jana Agosti 27,2023) unaoendelea kutekelezwa na Mkandarasi M/s Estim Construction Limited kwa gharama ya shilingi Bilioni 28.03 zilizotolewa na serikali.
“Ni rai ya Kamati ya Bunge kuwa soko hili ni la kimataifa hivyo Bodi na Menejementi ziwe na mpango wa uendeshaji soko kimataifa kama ilivyo lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kutoa fedha nyingi kujenga na kukarabati mradi huu wa kimkakati kwa nchi”, alisema Nyamoga.
Nyamoga alitoa ushauri kwa Shirika la Masoko ya Kariakoo kuwa na mfumo wa ukusanyaji na uchakataji wa taka wa kisasa ili kuepuka kero kwa wafanyabiashara na kuwa suala la udhibiti wa madalali liwekewe mkakati ili soko litakapofunguliwa wakulima wafanye biashara kwa faida na uwazi.
Kuhusu ugawaji wa vizimba na maeneo ya biashara, Kamati ya Bunge imeshauri Shirika la Masoko ya Kariakoo kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwepo kabla ya soko kuungua wapewe kipaumbele na kuwepo na uwazi wa waombaji wa nafasi za biashara hatua itakayosaidia kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Hawa Ghasia, alisema tayari maandalizi ya kuwarejesha waliokuwa wafanyabiashara wapatao 1,662 yanaendelea ikiwemo kuwahakiki na kuweka mpangilio mzuri wa biashara na kuwa soko litakapokamilika litakuwa na zaidi zitakazotangazwa kwa umma.
Ghasia aliwaeleza Wabunge hao kuwa katika soko jipya la Kariakoo mifumo madhubuti ya udhibiti wa majanga ikiwemo moto imewekwa pamoja na uwepo wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA itakayowezesha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha serikali inapata faida katika mradi huo.
Soko Kuu la Karikoo ambalo liliungua moto Julai 10 mwaka 2021 linakarabatiwa huku lililokuwa soko dogo likijengwa upya ambapo litakuwa na ghorofa nane, kati ya hizo mbili zipo chini ya usawa wa ardhi (basement) na sita juu ya usawa wa ardhi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilifanya ziara ya kikazi ya siku tatu jijini Dar es Salaam kwa kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (TARURA), Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART) na Shirika la Masoko ya Kariakoo (KMC).