Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Bunge ya Bajeti Yakagua Shughuli za Upakuaji Mafuta Dar es Salaam
Oct 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imefanya ziara katika maeneo yanayotumika kupakua mafuta kutoka kwenye Meli na kupima katika Bandari ya Dar es Salaam na Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Ziara hiyo ilifanyika tarehe 13 Oktoba, 2022 ikiwa na lengo  la kujihakikishia kuwa kazi za ushushaji wa mafuta na upimaji mafuta katika sehemu hizo  zinafanyika kwa ufanisi na Serikali inapata mapato stahiki.

Baada ya kufanya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo, aliipongeza Serikali kwa jinsi ilivyowekeza katika miundombinu ya ushushaji wa mafuta pamoja na mita za kupimia mafuta hayo ambazo kwa miaka ya nyuma zilikuwa hazipo na hivyo Serikali ilikuwa haipati mapato stahiki.

Alisema kuwa, mita hizo za kupimia mafuta  licha ya kuiwezesha Serikali kupata mapato inayostahili,  kampuni zinazoagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi pia zinapata uhakika wa kiasi cha mafuta ambacho wamekiagiza.

Vilevile alisema kuwa, Kamati hiyo ilifanya ziara katika Bandari ya Mtwara ambapo pia Wajumbe walishuhudia juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuiendesha sekta ya mafuta kwa ufanisi kwani mita za kupimia mafuta katika bandari hiyo zinafanya kazi vizuri na pia upanuzi wa bandari pamoja na sehemu za kuhifadhia mafuta unaendelea vizuri hali itakayofanya bandari hiyo kupokea mafuta kwa wingi zaidi. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi