Na Tiganya Vincent - RS Tabora
Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) mkoani Tabora kwa kauli moja wameridhia kuunganishwa kwenye Chama Kikuu cha Ushirika kwa ajili ya kuchukua Wilaya za Urambo na Kaliua ili kuanzisha chama kingine kipya cha maeneo hayo.
Hatua hiyo imefikiwa na viongozi kutoka Vyama vya Msingi (AMCOS) mbalimbali kwenye Mkutano Mkuu wa 25 ulifanyika jana mjini Tabora.
Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Tito Haule alisema uamuzi wa kuchukua baadhi ya wanachama wa WETCU na kuanzisha Chama kipya ni kurahisisha usimamizi wa vyama vya msingi na kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kuvunja Bodi ya WETCU kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Alisema kuwa WETCU itaendelea kubaki na usajili wake wa awali na itakuwa na Vyama vya Msingi (AMCOS) kutoka Uyui, Tabora Manispaa, Nzega na Sikonge.
Haule aliongeza kuwa kisheria kama Chama cha WETCU kingevunjwa ingechukua hata miaka miwili kuanzisha kingine na baada ya kufanyika ufilisi na ndipo chama kipya kianzishwe, ndio maana wameona ni vema kiendelee na usajili ule ule na kianzishwe kipya kitakacho hudumia Urambo na Kaliua.
Alisema kuhusu madeni yatabaki Chama cha WETCU na kile kipya cha kitakachoanzishwa kitaanza bila deni kama takwa la kisheria linavyohitaji ili kiwe na sifa ya kusajiliwa.
Haule alisema viongozi wanaweza kukutana na kupendekeza jina la Chama kipya au kinaweza kuitwa UKACU ili kuendelea na taratibu za usajili na kuahidi kutangaza Bodi ya Mpito ya Chama kipya tarajiwa hivi karibuni ili hatimaye ifikapo tarehe 16 Mwezi Juni mwaka huu kiwe kimesajiliwa.
Alisema baada ya usajili wanaweza kuitisha Mkutano wa uchaguzi kwa ajili ya kuwapata viongozi wao ili waweze kuwahi msimu wa mauzo ya tumbaku uliozindiliwa hivi karibuni wilayani Kahama.
Mmoja wa wakulima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Adamu Malunkwi alipongeza mapendekezo ya Serikali ya kupunguza ukubwa na WETCU kwa kuwa ndio ulikuwa kisababishi cha ubadhirifu kwa sababu ya viongozi kuwa na eneo kubwa na hivyo kushindwa kuvisimamia vema vyama vya msingi.
Alisema kuwa chama kitakachoanzishwa kitakuwa karibu na Vyama vya Msingi na hivyo kuwaondoa wakulima katika mateso na kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu unaotokana na ukubwa.
Mapema mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho.
Pia baada ya kuvunja Bodi ya WETCU alipendekeza igawanywe na iwe na vyama viwili vikuu kwa ajili kuwa Chama Kikuu cha Ushirika kitakachoweza kuzisimamia vizuri AMCOS kwa ajili ya manufaa ya mkulima.