[caption id="attachment_23324" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (katikati) akizungumza na ugeni kutoka Benki ya Kilimo ulipomtembelea Ofisini kwake Mkoani Kagera. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila na Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani (kulia).[/caption]
Na mwandishi wetu, Kagera
Mkoa wa Kagera umeweka bayana nia yake ya kuchangamkia fursa za mikopo nafuu inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuwasaidia katika kuendeleza shughuli za kilimo na uzalishaji mkoani humo.
Akizungumza wakati ugeni kutoka TADB ulipotembelea mkoani Kagera, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu alisema Mkoa wake upo tayari kutumia fursa za mikopo nafuu inayotolewa na TADB ili kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara mkoani humo.
[caption id="attachment_23325" align="aligncenter" width="750"] Ugeni kutoka Benki ya Kilimo wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa Wilaya na viongozi waandamizi wa Mkoa huo.[/caption]Aliongeza kuwa mkoa wa Kagera upo tayari kutumia fursa za uwepo wa Benki ya Kilimo ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini mkoani humo.
Mkuu wa mkoa huyo alisema kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa Benki ya Kilimo unalenga kutimiza dhamira ya Serikali ya kuwasaidia wakulima nchini kote kukabiliana na mapungufu kwenye kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.
“Kwa kuzingatia majukumu ya kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo, Mkoa wa Kagera upo tayari kufanya kazi bega kwa bega ili kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo mkoani kwetuu,” alisema.
Alitoa wito kwa wakulima wa mkoa wa Kagera kuchangamkia mikopo nafuu ya Benki ya Kilimo ili wajiongeze tija katika kilimo chao kwa kuwa Benki hiyo ipo kwa ajili ya kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Akizungumzia dhima ya safari hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila alisema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Bibi Kurwijila aliongeza kuwa Benki ya Kilimo ipo kwa ajili ya kutoa mikopo ya gharama nafuu na uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika kilimo nchini
Aliongeza kuwa Benki ya Kilimo imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa kilimo cha mazao yote yatokanayo na mbogamboga na matunda ili kuongeza tija kwa wakulima nchini kote.
“Benki ya Kilimo ni taasisi ya Serikali ambayo imenzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini hivyo tumejipanga katika kusaidia kutatua changamoto hizo,” alisema.
Kwa mujibu wa malengo ya uanzishwaji wa Benki hiyo ufinyu wa upatikanaji wa fedha mikopo ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa pamoja na riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo.
Sababu nyingine ni mikopo kuelekezwa katika vipindi vya muda mfupi, masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumzia hali ya utoaji wa mikopo, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” alisema Chacha .