Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetoa siku saba kuanzia leo Agosti 24, 2023 kwa wananchi wanaomiliki au kuuza mavazi ya kijeshi au yanayoelekea kufanana na sare za Kijeshi kusalimisha mavazi hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amesema hayo leo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu katazo la kisheria la raia kuvaa, kumiliki au kuuza mavazi ya Kijeshi au yanayoelekea kufanana na sare za Kijeshi.
“Kwa muda sasa kumekuwepo na wimbi kubwa la baadhi ya wananchi wanaokamatwa au kuonekana wakiwa wamevaa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania au mavazi yanayofanana na sare za Kijeshi,” amesema Luteni Kanali Ilonda.
Amesema kuwa, inakatazwa kuvaa mavazi hayo ambayo ni pamoja na Kombati (Vazi la mabaka mabaka), Makoti, Tisheti, Suruali, Magauni, Kofia, Viatu, Mabegi na Kaptula zenye rangi zinazofanana au kushonwa katika mitindo ya Kijeshi.
“Katazo hilo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 99 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa (NDA) sura 192 Sheria namba 24 ya mwaka 1966 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002. Aidha, Kifungu cha 178 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 (Penal Code) na kifungu cha 6 cha Sheria ya Usalama wa Taifa, vinakataza raia kuvaa sare na mavazi ya Majeshi ya Ulinzi au yanayofanana,” amesema Luteni Kanali Ilonda.
Ameendelea kusema kuwa, zipo baadhi ya taasisi zinazowashonea watumishi wake sare za aina hiyo. Pia, wapo wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia kupitia katika maduka au maeneo yao ya biashara. Aidha, wapo baadhi ya wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu.
“Wapo baadhi ambao kwa kuyatumia mavazi hayo wamekuwa wakiwatapeli wananchi na wengine kufanya vitendo viovu ambao pia wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni Wajajeshi. Vitendo hivyo ni vya uvunjifu wa sheria za nchi, hivyo havipaswi kufumbiwa macho. Aidha, hali hii ikiachwa kuendelea inaweza kuhatarisha Ulinzi na Usalama wa nchi yetu,” amesema Luteni Kanali Ilonda.