Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JWTZ Wakabidhiwa Jukumu la Kulinda Ukuta Unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani
Apr 07, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_29959" align="aligncenter" width="723"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite ambapo amewaasa watanzania kuendelea kushikamana katika mapambano ya kiuchumi yanayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.[/caption]

Frank Mvungi, Maelezo Manyara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa watanzania kuendelea kushikamana katika mapambano ya kiuchumi yanayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

Kauli hiyo imeitoa leo wakati akizindua ukuta uliojengengwa kuzunguka eneo la migodi ya Tanzanite mirerani mkoani Manyara ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi yakiwemo madini  ya Tanzanite yanawanufaaisha wananchi wote na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“ Wapo waliosema kuwa ujenzi wa ukuta huu hautawezekana lakini leo Jeshi letu limethibitisha kuwa  yanayowezekana ulaya hata sisi kama Taifa tukiamua tunaweza na kukamilika kwa ukuta huu ni kielelezo tosha” Alisisitiza Mhe. Rais  Dkt. Magufuli.

Akifafanua Rais Magufuli amesema kuwa Serikali itajenga miundo mbinu yote muhimu katika eneo ikiwemo barabara  ili kuchochea ukuaji wa biashaara ya madini ya Tanzanite ambapo kutakuwa na utaratibu rafiki kwa wachimbaji wote ili Serikali iweze kupata mapato stahiki na wachimbaji wanufaike.

Akitolea mfano Rais Magufuli amesema kati ya makampuni 1700 ni makampuni 25 tu yaliyokuwa yakilipa kodi hali iliyochochea upotevu wa mapato ya Serikali kwa muada mrefu hali iliyozorotesha maendeleo katika eneo hilo na katika Taifa kwa ujumla.

“ Madini haya ni mali yetu hivyo ni lazima tuilinde kwa gharama yoyote na sasa nakuagiza mkuu wa majeshi (CDF) kuanzia sasa ukuta huu utalindwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na sio SUMA  JKT wala mtu mwingine yoyote” Alibainisha Dkt. Magufuli.

Katika eneo hili kutakuwa na Kituo cha pamoja cha kutolea huduma, mabenki na huduma zote zitakowezesha wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na uuzaji wa madini hayo kwa kuwa mnada wa madini hayo utakuwa ukufanyika katika eneo hilo la mirerani na si kwingineko kama ilivyokuwa awali.

“ Tunapozuia wizi wa Tanzanite, dhahabu, wizi wa wanyama wetu, wahusika hawawezi kufurahia na hawa ni watu wenye uwezo mkubwa hivyo uzalendo katika kulinda rasilimali zetu ndio utakaosadia kama vijana walioshiriki kujenga ukuta walivyoonyesha mfano wa uzalendo wao kwa vitendo kwa kushiriki katika ujenzi wa ukuta huu” Alisema Dkt. Magufuli na kusisitiza.

Pia Rais Dkt. Magufuli alimpongeza mgunduzi wa madini ya Tanzanite mzee Jumanne Ngoma na kutoa shilingi milioni mia moja kwa ajili ya matibabu kwa mgunduzi huyo ikiwa ni ishara yakutambua mchango wake katika maendeleo ya Taifa kufuatia ugunduzi huo alioufanya mwaka 1967 katika eneo la mirerani.

Mkoa wa Manyara umeshapokea zaidi bilioni 6 kwa ajili ya mpango wa elimu bure na pia kuna miradi ya upanuzi wa vituo vya afya, zahanati na mwaka huu wa fedha zaidi ya Bilioni 1.6 zimetwngwa kwa ajili ya ujenzi wa hosipitali ya  rufaa ya mkoa, utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani  ya zaidi ya bilioni 2.4 katika eneo la mirerani unaendelea na wilaya ya Simanjiro kwa ujumla ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuondoa adha ya upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Anjellah Kairuki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imeshaandaa kanuni zitakazosimamia uendeshaji wa eneo hilo lenye ukuta wa kuzunguka migodi ya Tanzanite ili dhamira ya kujengwa kwa ukuta huo itime.

“ Tayari katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita tumeona tofauti ya makusanyo ya mapato yanayotokana na madini ya Tanzanite ukilinganisha na miakaliyopita ambapo kwa miezi mitatu tumekusanya zaidi ya milini mia saba” Alisisitiza Kairuki.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa muda uliopangwa katika kutekeleza mradi huo ni miezi sita ambapo kutokana na umahiri na uwezo wa Jeshi mradi huo umetekelezwa kwa miezi mitatu tu.

Ujenzi wa ukuta huo ni Agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilolitoa mwezi Novemba mwaka 2017 wakati akizindua barabara ya KIA  mererani iliyojengwa kwa kiwango cha lami, vijana zaidi ya 2000 wameshiriki katika ujenzi wa ukuta huo wakiwa ni wale wa operesheni Magufuli na Operesheni Kikwete ambao wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa vitendo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi